Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makamba: Tuko tayari kufanyakazi na ATOGS

Pics Pg 9 Okt 06 Makamba: Tuko tayari kufanyakazi na ATOGS

Wed, 6 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati iko tayari kufanya kazi na Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) ili kuendelea kuwezesha wananchi kushiriki ipasavyo katika sekta hiyo.

Makamba alisema hayo juzi alipofanya mazungumzo na Wajumbe wa Bodi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Abdulsamad Abdulrahim, baada ya Jumuiya hiyo kufika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma kwa ajili ya kueleza malengo yake na masuala mengine  yanayohusu jumuiya hiyo ambayo ina wanachama takribani 128.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja; Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Dk. James Mataragio na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA), Charles Sangweni. 

“Sisi tuko tayari kufanya kazi na ninyi, kwani tunaamini wananchi wengi wanaweza kunufaika na fursa zinazotokana na hii sekta kutokana na uwepo wa jumuiya hii ambayo inawapa wananchi taarifa mbalimbali kuhusu fursa zilizopo pamoja na  kuwaunganisha na mamlaka mbalimbali pamoja na wafanya maamuzi,” alisema Waziri Makamba.

Alisisitiza kuwa Wizara ya Nishati na taasisi zake zitaunga mkono taasisi au jumuiya ambazo zina malengo chanya ikiwamo ya kuwaunganisha wananchi na kuwapa fursa na taarifa zitakazowasaidia katika kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Wajumbe wa jumuiya hiyo waliushukuru uongozi wa Wizara ya Nishati kwa kuwapokea na kuwasikiliza na kueleza kuwa nia yao ni kushirikiana na serikali katika utaratibu wowote utakaopelekea wananchi wengi washiriki kwenye  shughuli za kiuchumi katika Sekta ya Mafuta na Gesi.

Chanzo: ippmedia.com