Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makali ya tozo yazua mjadala

Simu Tozoipo Makali ya tozo yazua mjadala

Sat, 20 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati wananchi wakilalamikia utitiri wa kodi ikiwamo mpya ya miamala ya fedha kupitia benki, wachumi wamependekeza kuanzishwa kwa vyanzo vipya ili kutanua wigo wa walipakodi na kuepuka kuvikamua zaidi vichache vilivyopo.

Hata hivyo, Serikali imesema kodi iliyowekwa katika miamala ya fedha kupitia benki ni sehemu ya bajeti yake iliyoidhinishwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23 na Bunge.

Julai Mosi mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kupitia gazeti la Serikali No.478 alitangaza kuanza utekelezaji wa kodi hiyo.

Lucy Kassim mkazi wa Mbeya, aliitaka Serikali kufikiria namna ya kupunguza hali hiyo ili kuepusha wananchi kurejea mtindo wa kutunza fedha kwenye vibubu na kudhoofisha ukwasi katika benki.

“Hatukatai kodi ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi, lakini kumekuwa na utitiri wa kodi. Siku za nyuma tulitumia M-Pesa, Tigo Pesa, Halo Pesa kama benki. Tulihifadhi akiba huko.

Wakaweka kodi sasa mlolongo huo wa kodi umeenda tena hadi benki. Yaani mimi kama mfanyakazi nimekatwa PAYE, sasa naamua kutunza kile kidogo kinachobaki, nacho wanakifuata huko benki wanakata kodi,” alisema.

Alisema Serikali inapaswa kubana matumizi yake na fedha zitakazobaki ndizo zitumike kutekeleza miradi lengwa.

Matata Mfunami, Jef Edward na Miriam Salehe, kwa nyakati tofauti, walisema kodi hizo zinatishia kuwatia hasara katika shughuli zao, kwa sababu fedha ile ile inakatwa zaidi ya mara moja.

“Hakuna kwa kukimbilia sasa tunaomba Serikali iangalie upya utaratibu huu, unazidi kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa chini,” alisema Jef Edward, mkazi wa Dodoma.

Wataalamu wa uchumi

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wataalamu wa uchumi wamependekeza mbinu itakayopunguza wingi wa kodi kwa wananchi.

Mtaalamu wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo alisema ufanisi katika shughuli za Serikali utafikiwa iwapo kodi zitalipwa.

Lakini, alisema hakuna namna yoyote ambayo Serikali itapata kodi nyingi pasina kutanua wigo wa mapato, jambo aliloeleza kuwa wengi hawaelewi maana yake.

Dk Kinyondo alifafanua kutanua wigo wa mapato haimaanishi kutoza kodi nyingi katika bidhaa moja, au kuongeza tozo katika chanzo kimoja.

Badala yake, alisema ni kutengeneza mazingira yatakayoifanya nchi iongeze walipakodi wapya, ambao awali haikuwa nao.

“Msingi wa kupata kodi nyingi ni kutanua wigo wa walipakodi kwa maana Serikali inapaswa itengeneze mazingira yatakayoibua au kuanzisha walipakodi wapya,” alisema.

Hatua ya kuongeza kodi katika chanzo ambacho tayari kilishakuwa kinatozwa, alisema inasababisha kukidhoofisha, hakitakuwa na hatimaye kitakufa kabisa.

Kwa mujibu wa Dk Kinyondo, kufa kwa chanzo cha kodi kunapunguza wigo wa mapato na hivyo, badala ya kuongeza makusanyo, unapunguza na uchumi wa Taifa unadhoofika.

“Serikali inapaswa kufikiria mlipa kodi mpya na huyu anapatikana kwa uchumi kukua, ukiweka mazingira mazuri ya biashara, aliyekuwa halipi kodi biashara yake itakua na ataanza kulipa kodi hivi ndivyo vyanzo vipya,” alisema.

Mtazamo wa mchumi huyo unaungwa mkono na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti (Repoa), Dk Donald Mmari aliyesema kutanua wigo wa kodi, kunapunguza kiwango na idadi ya tozo kwa chanzo kimoja.

Kwa bahati mbaya, alisema Tanzania ina walipakodi wachache na hivyo Serikali inapaswa kujikita katika kuwaongeza wapya na kuwafikia wale wanaostahili kulipa.

“Kama utakuwa na walipakodi wengi maana yake hutalazimika kuwabana wachache watoe kikubwa. Hii itawafanya wakue na kadri wanavyokuwa na ndivyo kodi inaongezeka ukiwa na wengi wanaokuwa utajikuta uko mbali,” alifafanua.

Serikali yafunguka

Wakati wachumi wakipendekeza hayo, Serikali imesema kodi iliyowekwa katika miamala ya benki ni sehemu ya bajeti yake iliyoidhinishwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa mwaka 2022/23.

Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema kwa ujumla fedha zitakazopatikana zitakuwa sehemu ya bajeti ya Serikali na zitatumika katika shughuli zilizoidhinishwa kwenye wizara, mikoa, halmashauri, kata, mitaa na vijiji katika sekta mbalimbali.

“Miongoni mwa maeneo zitakapotumika ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, maji na barabara na utoaji wa ruzuku za elimu kwa shule za msingi na sekondari,” alisema.

Aliyataja maeneo mengine ni mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ikiwamo ujenzi wa masoko ya machinga.

Alipoulizwa iwapo Serikali inafikiria kuchukua hatua baada ya malalamiko ya wananchi, Tutuba alijibu wakati wa bajeti viwango vya tozo vilipunguzwa kwa asilimia 60.

Alisema kwa miamala isiyozidi thamani ya Sh3,000 kiwango cha chini cha tozo kilipunguzwa na kuwa Sh10, huku Sh4,000 ikiwa ni kiwango cha juu kwa miamala inayozidi thamani ya Sh3 milioni.

“Kama utakumbuka wakati wa bajeti, Serikali ilitangaza kupunguza viwango vya tozo kwa asilimia 60 na kufanya kiwango cha chini cha tozo kuwa Sh10 kwa miamala isiyozidi thamani ya Sh3,000 na kiwango cha juu kuwa Sh4,000 kwa miamala inayozidi thamani ya Sh3 milioni,” alisema Tutuba.

Imeandikwa na Suzy Butondo, Sharon Sauwa na Bakari Kiango.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live