Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makaa ya mawe yapaisha bandari ya Mtwara

66970c7ace53d7be436efd3b0198c9e4.PNG Makaa ya mawe yapaisha bandari ya Mtwara

Tue, 2 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuongezeka kwa biashara ya makaa ya mawe kutoka Kusini mwa Tanzania kumeipa Bandari ya Mtwara ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini maisha mapya.

Pamoja na ongezeko hilo linalofanya bandari hiyo kuwa katika orodha ya bandari zinazopokea meli kubwa kwenda Ulaya na Bara la Asia katika ramani za vyombo vya baharini, maboresho yaliyopo yameleta fikra mpya kwa watumiaji wa bandari.

Hatua za makusudi za kupanua na kuifanya bandari hiyo yenye asili ya kina kirefu cha maji kuwa ya kisasa imeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wake na ufanisi wa kuhudumia mizigo.

Uwekezaji wa kimkakati wa serikali katika uboreshaji wa Bandari ya Mtwara umegeuza bandari hiyo kuwa tegemeo la usafirishaji wa mizigo kwenda na kutoka mikoa ya Kusini mwa Tanzania na mataifa jirani.

Maana ya uwekezaji huo unaonekana katika ongezeko la shehena na mapato kama takwimu za mwaka wa fedha uliopita zinavyoonyesha Katika kipindi cha miezi michache shehena ya mizigo inayopita Bandari ya Mtwara, hususani makaa ya mawe, imepanda kwa kiasi kikubwa, huku makusanyo ya mapato yakipanda pia.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mhasibu wa Bandari ya Mtwara, Teddy Kalolon, ukusanyaji wa mapato uliongezeka kutoka Sh bilioni 14 mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh bilioni 23 mwaka wa fedha 2021/22, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 64.2.

Usafirishaji wa makaa ya mawe kupitia Bandari ya Mtwara umeongezeka na hadi kufikia Juni mwaka huu tani 59,960 za makaa ya mawe ya Tanzania kutoka mkoani Ruvuma yalisafirishwa moja kwa moja hadi Amsterdam, Uholanzi ndani ya meli ya MV ETG Southern Cross.

Ilikuwa ni ongezeko kidogo kutoka rekodi ya awali ya mauzo ya makaa ya mawe ya tani 59,815 iliyosafirishwa hadi Misri mnamo Machi 4, mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za usimamizi wa mizigo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika Bandari ya Mtwara, kati ya Oktoba mwaka jana na Aprili mwaka huu, bandari hiyo ilihudumia tani 245,732.30 za makaa ya mawe yaliyosafirishwa kwenda nchi mbalimbali; India (tani 145,917.3), Misri (tani 59,815) na Senegal (tani 40,000).

Ikiwa na mifumo mipya ya kuhudumia shehena, bandari hiyo inazidi kutambua uwezo wake wa kuwa bandari ya kimkakati kwa nchi; na kwa kuunganisha sehemu ya Kusini mwa Tanzania na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi nyingine duniani.

Tayari Chama cha Wachimbaji Madini cha Bonde la Ufa kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Afrika Kusini na Uingereza wameeleza nia yao ya kutumia Bandari ya Mtwara kupitisha takribani tani 110,000 za makaa ya mawe kila mwezi kutoka Tanzania hadi Asia na duniani kote.

Chama cha Wachimbaji wa Bonde la Ufa kimesema kinafanya mazungumzo na uongozi wa Bandari ya Mtwara kuhusu mpango wa usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda katika masoko ya nje kupitia Bandari ya Mtwara.

Chama hicho kinaamini kuwa Bandari ya Mtwara ina vifaa vya kutosha vya kuhudumia shehena zao za makaa ya mawe kwani imeboresha miundombinu na kujivunia vifaa vya kisasa ili kuhakikisha usafirishaji wa shehena zao za makaa ya mawe kwa ufanisi na kwa wakati.

Selim Kaymak, mwekezaji kutoka Afrika Kusini na Mkurugenzi wa Kampuni ya Alpha Resources Mining aliielezea Bandari ya Mtwara kuwa ni bora kwa uwekezaji wa aina yoyote wa madini baada ya kufanyiwa upanuzi mkubwa.

“Bandari ya Mtwara ni muhimu sana kwa uwekezaji wa aina yoyote wa madini hata katika mikoa na maeneo mengine...tunashukuru sana kwa kukaribishwa na msaada wenu kutokana na majadiliano ambayo tumekuwa nayo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa ImpoExpo Logistics, Eurutunu Malamia, Chama cha Bonde la Ufa pamoja na wawekezaji hao wanapanga kusafirisha tani milioni 1.2 za makaa ya mawe kutoka Tanzania kwenda Asia na maeneo mengine duniani kila mwaka.

Malamia aliongeza kuwa ImpoExpo imeridhishwa na uwezo na ufanisi wa Bandari ya Mtwara na kuishukuru serikali kwa jitihada kubwa za kuboresha bandari hiyo ambayo inaelezwa kuwa ni bandari ya asili.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdilla Urio alieleza kufurahishwa na mipango ya chama hicho na wawekezaji wa kutumia Bandari ya Mtwara, akisema mipango hiyo itaboresha shughuli za bandari hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Nicodemus Mushi aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiunga mkono Mamlaka hiyo ili kufikia malengo yake.

Mushi alisisitiza dhamira ya Mamlaka ya kuboresha miundombinu, huduma na ufanisi katika bandari za baharini na nchi kavu sambamba na dhamira yake ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa majini kinachopendelewa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Pamoja na kufurahishwa na ongezeko la shehena na mapato ya kuvutia katika Bandari ya Mtwara, Mushi alisema bandari hiyo ina mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya uchumi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania na uwepo wake unakuza uzalishaji wa ajira. Bandari ya Mtwara iliyojengwa kati ya mwaka 1948 na 1954 ni miongoni mwa bandari kuu tatu zinazosimamiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Nyingine ni Dar es Salaam na Tanga. Kutokana na eneo lake la kimkakati, bandari hiyo pia inatumika kama lango bora kwa ulimwengu wa nje kwa mauzo ya bidhaa na uagizaji wa bidhaa kwa baadhi ya maeneo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kama vile Msumbiji, Malawi na Zambia.

Kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa bandari hiyo, serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ilitekeleza mradi wa upanuzi kwa gharama ya Sh bilioni 157.8. Upanuzi huo ulihusisha ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na kina cha mita 13.5 na kuiwezesha bandari hiyo kuchukua meli kubwa zenye uzito wa tani 65,000.

Upanuzi wa eneo la kuhifadhia mizigo bandarini kufikia ukubwa wa mita za mraba 79,000. Awali bandari hiyo ilikuwa na yadi ya kuhifadhi yenye ukubwa wa mita za mraba 40,000 pekee.

Bandari ya Mtwara pia imeongeza uwezo wake wa kuhudumia mizigo kutoka tani 400,000 kwa mwaka hadi tani 1,000,000.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live