Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Stephan Ngailo, alisema juzi kuwa kati hizo tani 38,000 ni mbolea ya aina ya CAN ambayo itaingia kati ya Agosti 10 na 12.
Pia alisema tani 33,000 ni UREA ambazo zitaingia nchini kabla ya mwishoni mwa mwezi. Pia alisema tani 16 zingine za aina ya UREA zitaingia baadaye.
"Kwa hiyo ukijumlisha hapo kuna kama tani za UREA 50,000. Hiki ni kiasi kingi cha mbolea na kimsingi mbolea nyingi itaingia zaidi kwa hiyo niwatoe hofu wakulima kwamba mbolea itakuwapo,’’ alisema Ngailo.
"Na kwa habari ya bei serikali inaangalia namna ya kupunguza makali. Kwa hiyo serikali haijalala inafanya kazi kuhakikisha kwamba mkulima anapata mbolea kwa wakati na kwa bei ambayo anaweza akaimudu,” alisema.
Ngailo pia alisema kwa mikoa ya Iringa, Ruvuma na Njombe suala la upatikanaji mbolea linaridhisha kwa kuwa ina takribani tani 8000.
"Iringa kuna zaidi ya tani 1,000, Ruvuma kuna zaidi ya tani 2,000 na hapa Njombe kuna zaidi ya tani 5,000 na hii tunasema si msimu hasa kwa hiyo tuna uhakika kwamba mbolea itaendelea kuingia katika mikoa hii na upatikanaji wake hautakuwa na shida,” aliongeza.
Ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo, mkurugenzi huyo alihimiza Watanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya mbolea.
Naye Meneja Mkuu wa Mtewele General Traders, Sady Mwang’onda, aliwatoa hofu wakulima kuwa maghala yao yana pembejeo za kutosha na kwamba kuna mbolea nyingine iko njiani.
"Tunajiandaa na msimu wa kilimo. Tuna magari mengi yanaleta mbolea kutoka Dar es Salaam kuja hapa na kwa kadiri msimu unavyozidi kusogea na sisi tutaendelea kuleta mbolea ya kutosha ili kuhakikisha mkulima hapati shida ya kuipata,” alisema.