Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa kufanya marekebisho katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa yakileta changamoto katika shughuli za uwekezaji na biashara.
Waziri Mkuu amesema kuwa serikali imefuta kodi na tozo zaidi ya 374 zilizokuwa ni kero katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo, uvuvi, maliasili na misitu pamoja na kufanya maboresho ya kisera ya mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuwezesha uwekezaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo katika hafla ya Uzinduzi wa Taarifa za Maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara ya Nyenzo za Usimamizi wa Uwekezaji Nchini inayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa serikali katika kuboresha mazingira ya biashara nchini imeanzisha idara ya viwanda, biashara na uwekezaji katika mamlaka ya serikali za mtaa zote 184 pamoja na kuondoa mwingiliano wa majukumu kwa taasisi mbalimbali ili kupunguza kero kwa wafanyabiashara.