Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuhudumia wawekezaji na kuifanya ajenda hiyo kuwa ya kudumu, ikienda sambambana na kutangaza fursa za uwekezaji nchini. ili kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji wa nje na ndani, na kuongeza pato la taifa.
Majaliwa amebainisha hilo jijini Dar es Salaam katika Uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa kuhudumia wawekezaji kwa dirisha moja, uliotengenezwa na wataalam wa ndani, Kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, (Tanzania Electronic Investment Window) TeIW pamoja na Muongozo wa Kituo cha Uwekezaji wa Kuwasajili watoa huduma. uliofanyika usiku wa kuamkia leo Septemba 26, 2023 katika ukumbi wa Mlimani City.
Amesema mfumo huo utasaidia kuondoa malalamiko ya udanganyifu kutoka kwa wawekezaji dhidi ya watoa huduma, kuongeza ajira nchini na kuepuka uwepo wa vishoka wanaotumia fursa hiyo kuwatapeki watu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema matarajio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kujenga uchumi wa kisasa wa viwanda na kudimisha imani kwa wawekezaji ili kuvutia uwekezaji mkubwa, hivyo wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa adau wote katika kufanikisha hilo.