Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa awataka Watanzania waishio nje ya nchi kushawishi wawekezaji

15326 Pic+majaliwa TanzaniaWeb

Mon, 3 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio nje ya nchi  wahakikishe wanashiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi yao  kwa kushawishi wawekezaji wenye mitaji mikubwa waje kuwekeza nchini na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inaamini Tanzania itapata maendeleo makubwa ya kiuchumi endapo wananchi wake watatekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi tu’.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu leo, Septemba 2, 2018 inasema Majaliwa aliyasema hayo jana jioni wakati akizungumza na Watanzania waishio nchini China kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo jijini Beijing.

Alisema nchi zote zilizoendelea zilihakikisha wananchi wake wanaelewa na kutekeleza matamko yanayowahamasisha kufanya kazi, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahamasisha Watanzania popote walipo kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu.’

Waziri Mkuu alisema China ambayo imefanikiwa kuwa moja kati ya nchi zenye nguvu  kubwa ya kiuchumi duniani, imefika hapo kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na wananchi wake walioamua kuunga mkono juhudi za Serikali yao kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi wakiwa ndani au nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Watanzania waishio nje ya nchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu hasa biashara ya dawa za kulevya ambayo inachafua jina na heshima ya nchi yao kimataifa.

“Tanzania ni nchi nzuri na inaheshimika duniani, nawasihi mnaoishi nje muachane kabisa na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa sababu inalitia doa Taifa na adhabu yake katika baadhi ya nchi ni kifo,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema mwelekeo wa Tanzania kwa sasa ni diplomasia ya kiuchumi (economic diplomacy), hivyo Watanzania waishio nje wanapaswa kuwa wabunifu, makini katika kutafuta fursa zenye manufaa kwa nchi yao.

Alisema Diplomasia ya Uchumi si kupeleka Tanzania wawekezaji tu bali wawekezaji katika viwanda ambavyo kila vinapojengwa vinachangia kuinua uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki aliwaasa vijana kuitumia teknolojia ya mawasiliano na mitando ya jamii kutafuta habari na taarifa muhimu hasa nafasi za masomo ili kujiendeleza kielimu.

Chanzo: mwananchi.co.tz