Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ataka msisitizo zaidi diplomasia ya uchumi

Majaliwa Pic Data Majaliwa ataka msisitizo zaidi diplomasia ya uchumi

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuweka msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na kuhamasisha upatikanaji wa masoko wa bidhaa za ndani na uwekezaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, alipokutana na mabalozi ofisini kwake jijini Dodoma na kuongeza kuwa maboresho ya sera na mfumo wa uwekezaji uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Alisema Tanzania inahitaji wawekezaji wenye tija watakowekeza kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, madini na maliasili.

“Tunataka uwekezaji wenye tija ili kuimarisha uchumi wetu, pia tunataka wawekezaji watakaozalisha bidhaa hapa nchini kwa kutumia malighafi zetu…

“Nchi yetu ni moja kati ya mataifa ambayo jiografia yake imekaa kimkakati, tuna masoko kutoka jumuiya mbalimbali ikiwemo SADC na EAC, hata mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tunazo ndege, bandari na sasa tunaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye sekta ya nishati,” alisema Waziri Mkuu.

Amewataka mabalozi hao kuandaa makongamano na vikao vya pamoja vya kibiashara kati ya wafanyabiashara wa nchi wanazoziwakilisha na sekta binafsi wa nchini Tanzania.

“Nendeni mkatafute masoko ya bidhaa zetu za ndani, shirikini kwenye maonesho yanayoandaliwa, ili mtangaze bidhaa zetu, tunataka wakulima wetu wanufaike kwa kupata masoko kutoka kwenye nchi mnazokwenda, ” alisema.

Mabalozi aliokutana nao ni Balozi Caroline Chipeta (Uholanzi), Balozi Simon Sirro (Zimbabwe) na Balozi Luteni Jenerali Mathew Mkingule (Zambia).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live