Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa asema mnada wa kahawa kufanyika Kagera

21233 Majaliwa+pic TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukoba. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mfumo mpya wa kununua kahawa unaendelea kuboreshwa na kuanzia msimu ujao, mnada utafanyika mkoani Kagera badala ya kusafirishwa hadi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kama ilivyo sasa.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wafanyabiashara pamoja na wadau wa zao la kahawa baada ya kuwasili mjini Bukoba kwa ajili ya ziara ya kikazi mkoani Kagera.

Alisema hakuna sababu tena ya mnada wa kahawa ya Kagera kupelekwa mbali na kwamba hatua hiyo itaokoa gharama mbalimbali zinazobebwa na mkulima.

Alisema wanunuzi kuanzia msimu ujao watapaswa kwenda Kagera kwa ajili ya mnada huo.

Kuhusu vyama vya ushirika na madeni, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa vyama vyama hivyo kutumia vizuri rasilimali za vyama hivyo na kwamba Serikali haitalipa deni lolote lililokopwa na vyama hivyo.

“Biashara ya kununua madeni yaliyokopwa na vyama vya ushirika haipo kwenye Serikali hii ya Awamu ya Tano, badala yake itawachukulia hatua wote waliohusika na ubadhilifu huo,” alisema Majaliwa.

Awaonya wafanyabasha

Waziri Mkuu aliwaonya wafanyabiashara dhidi ya kuwaibia wakulima kwa kununua kahawa mbichi ikiwa shambani maarufu kama butura.

Alisema Serikali itachukua hatua kali kwa viongozi wa vyama vya ushirika ambao si waaminifu na wabadhilifu wa mali za ushirika.

“Tunahitaji wakulima wapate fedha,” alisisitiza na kubainisha kuwa Serikali itahakikisha wafanyabiashara wote, hususan wa mazao ya kilimo wanakuwa na mfumo sahihi wa ununuzi wa mazao utakaoongeza tija kwao na kwa wakulima.

Alisema kwa sasa Serikali inataka kuondoa mfumo uliopo wa vyama vya ushirika kufanya biashara na badala yake jukumu hilo libakie kwa wafanyabiashara.

Aliwataka wafanyabiashara hao waihakikishie Serikali kwamba watanunua kahawa yote iliyopo kwa wakulima pamoja na vyama vya ushirika.

Awali, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alisema mfumo rasmi wa kununua kahawa umekuja na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na zao hilo kutochukuliwa haraka kutoka kwa wakulima na kwenye maghala hali ambayo ilisababisha mzunguko mdogo wa fedha.

Aidha, alisema uzalishaji wa kahawa umekuwa mkubwa kwa nchi zinazolima zao hilo na kusababisha bei kushuka jambo alilosema halikuwa kutokea kwa miaka 12 iliyopita.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema pamoja na umuhimu wa zao la kahawa, inatakiwa kufanyika uwekezaji katika maeneo mengine kama viwanda vya maziwa ili kukuza uchumi.

Chanzo: mwananchi.co.tz