Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa akataa vishoka kwenye miradi ya maendeleo

Serikali Kufufua Viwanda Vya Korosho   Majaliwa.png Majaliwa akataa vishoka kwenye miradi ya maendeleo

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wathamini wote wawe waadilifu, wenye weledi na wazingatie miiko ya taaluma katika kazi zao za kila siku.

Majaliwa ameyasema hayo Novemba 9, 2023 akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wathamini uliofanyika mjini Dodoma.

Amesema, wathamini ni watu muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya Taifa hivyo wanapaswa kuwa waadilifu na kuzingatia thamani halisi ya ardhi, jengo au chochote kinachofanyiwa uthamini.

“Kazi ya uthamini si ya wababaishaji au vishoka, hivyo basi kila mthamini hana budi kuthamini na kuheshimu taaluma yake,”amesema Majaliwa na kuongeza

“Wapo baadhi ya wathamini ambao si waadilifu kwa kushirikiana na watendaji wengine hutoa makadirio ambayo hayawiani na thamani halisi. Vitendo hivyo husababisha kupoteza mapato ya Serikali lakini pia kuwanyima haki wale wanaostahili kupata haki,”amesema.

Aidha, Majaliwa amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hususani wathamini washirikiane na sekta binafsi kufanya kazi za uthamini.

“Tumieni fursa ya uwepo wa wathamini binafsi ili kutoa huduma bora na ya haraka hapa nchini, kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza maagizo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya ushirikishaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa,”amesema.

Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda amesema kuwa uthamini wa fidia ni ufunguo wa maendeleo na mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa kuwa unawezesha wawekezaji kupata ardhi na kuwekeza mitaji yao.

Amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wathamini nchini imejipanga kuhakikisha shughuli zote za uthamini zinaboreshwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live