Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa akaribisha wafanyabiashara kutoka Korea Kusini

11987 MAJALIWA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 23 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba wafanyabiashara kutoka Korea Kusini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Majaliwa amesema hayo leo Julai 23, 2018 akifungua jukwaa la kibiashara kati ya Tanzania na Korea Kusini jijini Dar es Salaam. Jukwaa hilo limehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-Yon.

Amesema Tanzania ina vivutio vingi ikiwamo zikiwamo hifadhi za Taifa, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Bahari ya Hindi na maziwa Victoria na Tanganyika.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema uwapo wa amani na utulivu ndiyo chanzo cha uwekezaji Tanzania.

"Tunakaribisha uwekezaji kutoka Korea Kusini katika sekta ya viwanda lakini fukwe za bahari inayoanzia Pwani ya Tanga hadi Mtwara zaidi ya kilomita 1,200," amesema.

Waziri Mkuu Lee ameshukuru ushirikiano baina ya Tanzania na Korea Kusini akisema utaendelea kudumishwa ili uwe wenye tija kwa mataifa haya mawili.

Amesema Korea Kusini iko tayari kushirikiana na Tanzania katika nyanja za afya, elimu, sayansi na miundombinu kama alivyoombwa na Rais John Magufuli kuangalia namna ya ushiriki wao kwenye ujenzi wa reli ya kisasa.

Waziri Mkuu Lee amepongeza ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambao Benki ya Dunia imeutambua hivyo kulifanya Taifa kuwa miongoni mwa nchi 10 ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Lee yupo nchini tangu juzi Julai 21, 2018 kwa ziara ya kiserikali kwa mwaliko wa Waziri Mkuu Majaliwa. Anatarajia kuondoka leo.

Chanzo: mwananchi.co.tz