Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ageuka mbogo awashukia TBS, TICTS

Majaliwa Pc Data Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

Mon, 11 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kampuni ya kimataifa inayoshughulikia upakuaji wa makontena ya mizigo bandarini (TICTS) kupunguza muda wa upakuaji.

Majaliwa alitoa maelekezo hayo juzi, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utendaji kazi kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Alisema Serikali inataka kumaliza urasimu unaolalamikiwa ili kuvutia wateja wengi zaidi.

“Kulingana na maelezo suala la ukaguzi wa magari unaofanywa na TBS hauna uhusiano, ana shughuli za bandari, lakini watu wanalalamika kuwa hapa bandarini kuna urasimu, nafikiri watu wasiilaumu bandari,” alisema Majaliwa wakati wa ziara yake katika eneo linalojengwa kituo cha ukaguzi wa magari.

Alisema TBS wanapaswa kuangalia viwango vya magari yanayoingia nchini ili kuhakikisha Tanzania haiwi dampo la magari yasiyo na ubora, lakini kama mtu ameridhia gari lake kama lilivyokuja asilazimishwe kuliacha hapo, badala yake apewe muda wa kuhakikisha anafanya matengenezo.

Majaliwa alisema magari mengine yanahitaji matengenezo madogo kama kubadilishwa tairi au mchubuko kwenye boda, mteja hatakiwi kuzuiliwa, maana wengine unakuta wanakaa mbali, kumuacha akae hapa mpaka amalize matengenezo ni kumuongezea gharama.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga alimwambia Waziri Mkuu kuwa wao hukagua magari baada ya kuwa yamemaliza mchakato wote wa kibandari na mamlaka nyingine, hivyo kwa namna yoyote hawasababishi usumbufu bandarini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka TICTS kuongeza ufanisi wao kwa kuhudumia meli haraka, akisema licha ya kampuni hiyo kuwa na vifaa vya kisasa, inachukua muda mrefu kupakua meli sawa na bandari ya Dar es Salaam ambayo haina vifaa, jambo linalohitaji uangalizi wa karibu.

“Kwa nini wakati mwingine meli zinakaa muda mwingi zaidi hapa kuliko Bandari ya Dar, es Salaam, tutaiangalia kwa karibu TICTS kadiri ya mkataba wetu, kwani wakati tunahuisha mkataba 2017 kuna mambo tulikubaliana ya kuboresha, nafikiri kuna cha kufanya hapa na hilo namwachia Waziri (Waziri wa Uchukuzi),” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema Serikali inataka ushushaji wa meji moja uwe chini ya siku 6, ili kuvutia wateja zaidi na TICTS itaangaliwa ikionekana ufanisi wake hauridhishi Serikali itaangalia cha kufanya.

“Kuna wawekezaji wengi wanaotaka kuwekeza katika bandari hii, kama utendaji wao hauridhishi tutaangalia cha kufanya,” alisema Majaliwa. Kwa pamoja Waziri Mkuu aliagiza taasisi zote zinazofanya kazi bandarini kufanya kazi saa 24 na kama kuna upungufu wa vitendea kazi na rasilimali watu viongezwe, ili kuongeza ufanisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live