Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aeleza kahawa itakavyouzwa nchini

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kuanzia sasa minada yote ya kahawa itafanyika kwenye maeneo yanayolima zao hilo.

Akizungumza na wadau wa kahawa katika ukumbi wa Jimboni wilayani Mbinga mkoani Ruvuma juzi, Majaliwa alisema maeneo hayo yamegawanywa katika kanda za Moshi, Kagera, Mbinga na Songwe.

Alisema hakutakuwa na sababu ya mkulima wa Kagera kukimbizia kahawa yake nchini Uganda.

“Siku ya mnada Mganda aje Kagera apite mpakani kwa utaratibu uliowekwa nchini, aseme amekuja kununua kahawa, tutamruhusu na watamsindikiza aje kununua kahawa, sisi atupe fedha yetu achukue kahawa aende zake,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema lengo la kufanya minada hiyo katika maeneo yanayolima kahawa ni kuongeza uwazi katika biashara hiyo na kuwawezesha wakulima kujua bei ya mnada na kulipwa kwa wakati.

Waziri Mkuu alisema Mbinga ni makao makuu ya kanda ya kilimo ya uzalishaji kahawa, hivyo mnada utafanyika hapo.

Alisema wakulima wa Mbinga hawatakuwa na haja ya kupeleka kahawa yao Namagoma ili iende Malawi.

“Siku ya mnada iwe wazi na itangazwe mapema, mtu wa Malawi aje tena apande meli tumeshaitengeneza, anunue kahawa apeleke kwao.”

Alisema kwa kufanya hivyo, bei ya mnada kila mkulima ataijua siku hiyo na Bodi ya Kahawa inatakiwa kusimamia minada yote, jambo litakaloleta uwazi katika ununuzi wa zao hilo na kuondoa manung’uniko ya wakulima.

Waziri Mkuu alisema mkulima anaruhusiwa kupeleka kahawa katika mnada wowote nchini ilimradi azingatie sheria na taratibu.

Alisema Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo ili kila mmoja anayehusika akiwamo mkulima aweze kunufaika na kuongeza tija.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema kuanzia sasa kahawa yote itakayozalishwa nchini ni lazima iongezwe thamani na hakuna itakayokuwa na maganda itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.

Pia, alipiga marufuku usafirishaji wa kahawa isiyokobolewa nje ya mipaka.

“Lazima kahawa yetu iongezewe thamani ndipo ipelekwe katika masoko ya nje ili iuzwe kwa bei nzuri, hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na kulinda uwekezaji wa viwanda uliofanyika nchini,’’ alisema Majaliwa.

Aliziagiza halmashauri zote zinazolima zao hilo kuwa na kitalu chenye miche zaidi ya 200,000 ifikapo Februari, mwaka huu.

Akizungumzia madeni ya wakulima, Waziri Mkuu aliagiza watendaji wote wa vyama vya msingi (Amcos) waliohusika watafutwe ili walipe.

“Kwa sasa Serikali haina taratibu za kununua madeni ya chama chochote cha ushirika. Kuendelea na utaratibu huo kunachochea viongozi wa ushirika kufuja mali. Lazima watambue ukifuja fedha za wanaushirika, Serikali iko na wewe,” alisema.

Alisisitiza kuwa hawatarudi nyuma kuwasimamia wakulima nchini ili nao waweze kunufaika na kazi kubwa wanazofanya.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Amcos kuhakikisha kuwa wakulima wote wanasajiliwa na taarifa zao ikiwemo ukubwa wa mashamba, kiasi cha uzalishaji na mahali walipo zinatunzwa vizuri kwenye kompyuta.

Pia, alimwagiza mrajisi msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma kuzikagua Amcos zote na kujiridhisha kama ziko hai na zenye tatizo la uongozi aitishe uchaguzi.

Kwa upande wao, wadau walifurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kusimamia zao hilo kwa karibu na hasa baada ya kutangaza minada yote ya kahawa kufanyika katika maeneo yao na kwa uwazi.



Chanzo: mwananchi.co.tz