Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aagiza Dodoma kujenga masoko ya machinga mengi

Majaliwa Pic Datafff Majaliwa aagiza Dodoma kujenga masoko ya machinga mengi

Thu, 10 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kukaa na machinga ili kukubaliana maeneo mengine ya kujenga masoko ya kisasa ya kufanyia biashara katika Jiji hilo.

Majaliwa ameyasema hayo Machi 9, 2022 wakati alipotembelea ujenzi wa majengo ya biashara ya machinga (Machinga complex) inayojengwa katika eneo la Bahi Road.

Majaliwa amewapongeza mkoa, halmashauri ya jiji kwa kujenga majengo hilo la kisasa ambayo yatakuwa mfano kwa kwa nchi nzima.

“Tutafute maeneo mengine ya kujenga masoko haya ili tuwe na masoko kama haya ya wafanyabiashara ndogo ndogo mengi yenye uziri kama hili leo,”amesema.

Majaliwa amesema Serikali imezungumza na mabenki nchini ambayo yamekubali kuweka viwango vya mitaji ya wafanyabiashara wadogo ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi yao.

Aidha, amewataka wakuu wa wilaya wa Mkoa wa Dodoma kuwasaidia machinga kuunda vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) ili waweze kupata mikopo kutoka kwa taasisi za fedha nchini.

Pia Majaliwa ameagiza kukamilika mapema kwa ujenzi wa soko hilo ili machinga hao waweze kuingia na kufanya biashara katika maeneo mazuri.

Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Tawala za Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amesema kati ya Sh5 bilioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuboresha maeneo ya kufanyia biashara kwa machinga, jiji la Dodoma limepelekewa Sh500 milioni.

“Sisi tunaiita ni mbegu ofisi ya Rais tutaongea na wadau wa maendeleo kuona namna tunavyoweza kutumia mbegu hii iweze kuzaa mbegu nyingine. Tumeshaanza mazungumzo na Serikali ya India ikipatikana tutaweza kuongezea,”amesema.

Amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka kwa kujiongeza baada ya kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuongezea katika ujenzi wa maeneo ya kufanyia biashara.

Naye Mtaka amesema vibanda hivyo vimejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya machinga na kwamba atakayeona vibanda ni vidogo itampasa kwenda kutafuta kibanda cha kukodi kwasababu atakuwa hakidhi vigezo vya kuwa kwenye eneo hilo.

“Sisi hatupendi kuitwa jiji la uchafu tumekubali kuwavumilia ili hawa wenzetu ili hawa watu tusiwavunjie. Tutakapomaliza ujenzi wa eneo hili mheshimiwa Waziri Mkuu hakuna atakayebaki mjini,”amesema.

Amesema watatoa wiki moja kwa machinga kuhamia kwenye eneo hilo mara baada ya ujenzi kukamilika na kwamba vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) watafika kwenye maeneo mbalimbali kusafisha usiku kwa wale watakao kaidi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amewataka machinga watakapokabidhiwa eneo hilo kuhakikisha kuwa wanalitunza kwa usafi na kulinda miundombinu.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema halmashauri ina machinga 3,500 wanaofanya biashara katika maeneo mbalimbali

Mafuru amesema eneo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kubeba wafanyabiashara 2,930 ambayo ni sawa na asilimia 88 ya wafanyabiashara waliopo kwenye Jiji la Dodoma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live