Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Wafanyabiashara tumieni fursa za Muungano

23e846e52d11c5c35c22679549286a4e Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

Mon, 25 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa pande zote mbili za Muungano watumie fursa za kibiashara ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wajengane kibiashara kabla ya kufikiria kutoka nje.

Alisema hayo jana alipomwakilisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango katika ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano katika Uwanja wa Maisara, Zanzibar.

Alisema Tanzania mbali na kuwa na soko kubwa la watu zaidi ya milioni 60 ndani ya Muungano, pia kuna soko kubwa zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hivi karibuni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilikaribishwa kuwa mwanachama wa saba wa EAC.

"Lakini pia litumieni vizuri soko la SADC (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika) pamoja na soko kubwa zaidi la nchi zote 54 za Afrika kupitia African Continental Free Trade Agreement," alisema Majaliwa.

Aliwataka Watanzania waendelee kujivunia na kutangaza mafanikio na maendeleo yanayotokana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

"Serikali zetu mbili zitaendelea kutekeleza maono ya viongozi wetu ya kuhakikisha changamoto za kifedha na za kikodi za pande za Muungano zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa manufaa ya serikali zetu zote mbili," alisema Majaliwa.

Kuhusu ufumbuzi wa hoja za Muungano, Waziri Mkuu alisema azma njema ya viongozi imeendelea kusimama imara kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

"Nyote ni mashahidi hivi karibuni tu tumetatuwa changamoto 11 ambazo kwa namna fulani zilikuwa zinakwaza wananchi wetu na bado kazi inaendelea kuzimalizia zilizobaki," alisema.

Alisema katika hoja zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja na suala la ajira katika Serikali ya Muungano na kwamba, Zanzibar ina asilimia 21 ya ajira zote zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majaliwa aliwataka vijana na Watanzania waendelee kulinda na kuzienzi harakati za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Uhuru wa Tanganyika ambavyo ni msingi wa Muungano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live