Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ufugaji wa ng’ombe nchini hauna tija hivyo wadau wa sekta hiyo wanatakiwa kuhamasisha ufugaji wa kisasa.
Majaliwa amesema ng’ombe milioni 33.9 nchini hawana mchango mkubwa kiuchumi ikilinganishwa na ufugaji wa Botswana.
Amesema Botswana wana mifugo wachache lakini wamekuwa na mchango mkubwa katika Taifa hilo.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 7,2022 wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Ushirikiano wa Wasindikaji na Wachakataji katika Tasnia ya Maziwa(TI3D), uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
“Ng’ombe wetu anatembea kutoka Maswa hadi Kilwa, wamesafiri umbali mrefu hadi miguu yote imekakamaa, sasa huyo Ng’ombe atazalisha maziwa kweli?,”amesema na kuongeza:
“Sisi tutakula nyama na kupongeza tu lakini wanaokula nyama kwa viwango itakosa soko.”
Amesema tayari kuna viwanda zaidi ya vitano lakini mifugo hiyo imekosa viwango vinavyohitajika katika viwanda hivyo.
“Ng’ombe wa kienyeji anazalisha kati ya nusu lita hadi 2 kwa siku lakini Ng’ombe wa Kisasa wanazalisha lita 20 hadi 30 kwa siku. Inabidi tuwaeleze wafugaji wetu hili,”amesema Majaliwa.