Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Serikali itaendelea kukuza uchumi

Majaliwa 177 Majaliwa: Serikali itaendelea kukuza uchumi

Thu, 18 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na uratibu wa uanzishaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika na tayari shilingi bilioni 15.7 zimekusanywa kutoka kwa Wanahisa kiasi ambacho ni sawa na asilimia 78.5 ya mtaji wa shilingi bilioni 20 zinazohitajika.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa Kongamano la Kumi la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililofanyika katika ukumbi wa Jenerali Venance Mabeyo, jijini Dodoma na kudai kuwa kuanzishwa kwa benki hiyo, kutaviwezesha vyama vya ushirika kupata mikopo yenye riba nafuu na kuendesha shughuli zake kwa tija.

Amesema Serikali imefanya maboresho ya kitaasisi kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi kwa kuunganisha Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Majaliwa ameongeza kuwa, pia Serikali imeunganisha Bodi ya Chai Tanzania na Umoja wa Wakulima Wadogo wa Chai ili kuwa na Bodi moja. Pia imehamishia shughuli za Bodi ya Pareto Tanzania kwenda kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko.

Amesema, "Kwa upande wa sekta ya mifugo na uvuvi, Serikali inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuunganisha Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa, kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji pamoja na Mamlaka ya Bidhaa na Miundombinu ya Mifugo."

Maboresho hayo, ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta hizo, hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau wa kongamano hilo kujadili namna bora ya kuiwezesha Tanzania kuwa sehemu ya maendeleo ya kilimo smati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live