Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia utafiti uliofanyika nchini na kupata mbegu mpya ya michikichi ambayo imeonesha mafanikio makubwa.
Mbegu hiyo bora ya michikichi aina ya TENERA inatoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na wakulima kwa takribani asilimia 90.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Kigoma wakati akihitimisha kikao chake na wadau wa zao la chikichi.
Amesema mtu yeyote anayetaka kulima chikichi nchini anaweza kufanya hivyo kwa sababu mbegu zipo.
“Tulianza kuzalisha mbegu mwaka 2018 na ilipofika mwaka 2020 tukaanza kupanda miche na leo tunaona matunda yanapatikana.”amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa “Twendeni mashambani, tutumie miche yetu iliyozalishwa ama na taasisi zetu, halmashauri zetu au vyama vya msingi (AMCOS). Tuna kazi ya kuhakikisha zao la chikichi linaenda kwa spidi kali zaidi.”