Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, lengo la Mkataba wa eneo huru la Biashara (AfCFTA) ni kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki katika kufanya biashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiufundi.
Akifungua Mkutano wa Pili wa Wanawake wafanyabiashara Barani Afrika unaofanyika Dar es Salaam, Tanzania, Waziri Mkuu amesema, Itifaki ya eneo huru ya biashara imelenga kuwawezesha wafanyabiashara wote wakiwemo wanawake na vijana fursa ya kuyafikia masoko yote barani humo bila vikwazo vyovyote.
Amesema, endapo fursa ya AfCFTA itatumika kama ilivyokusudiwa basi wafanyabiashara watapata maendeleo ya kasi na kukuza biashara zao kupitia masoko ya bidhaa mbalimbali barani humo.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa mbali na mkataba huo wa AfCFTA lakini pia kuna itifaki kadhaa zinazochagiza uwepo wa fursa kwa wanawake kufanya biashara na kuyafikia masoko mbalimbali ikiwepo itifaki ya Maputo ya maka 2003.