Serikali imetaka kufuatwa utaratibu wa uuzaji wa mazao yakiwemo ya chakula nje ya nchi huku ikisisitiza haijapiga marufuku wakulima kufanya hivyo.
Kauli hiyo inakuja baada ya mkwamo wa siku kadhaa wa malori 120 yenye shehena ya mahindi eneo la Himo mkoani Kilimanjaro kuelekea Kenya ambayo mkuu wa mkoa huo, Nurdin Babu alitaka yarudishe mzigo huo na kuuza nchini.
Hata hivyo, Julai 13, mwaka huu akiwa mkoani Mwanza, Rais Samia Suluhu Hassan alishauri wakulima wasiuze mazao ya chakula nje ya nchi, badala yake waiuzie Serikali ili iongeze hifadhi ya ndani. Kauli yake hiyo inatokana na kile alichoeleza kuna viashiria vya dunia kukabiliwa na njaa kwa siku zijazo.
“Kwa sasa nchi ina akiba ya chakula tani 200,000 hadi 250,000, tuna mpango wa kumwaga fedha kununua chakula, tunataka kuwa na hifadhi ya chakula tani 500,000 kwa mwaka huu tunaouanza, hivyo msiuze mazao nje kwa kuwa Serikali itayanunua,” alisema Rais Samia.
Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema Serikali haikupiga marufuku usafirishaji mazao nje ya nchi kwa biashara, bali imezuia kufanya hivyo bila kufuata utaratibu.
"Marufuku inayosemwa kwenye kusafirisha nje, ni kwa mazao yote ya kilimo ikiwemo chakula kwa wafanyabishara wasiofuata utaratibu. "Utaratibu unaotakiwa kufuatwa na mfanyabiashara ni kusajili kampuni yake hapa nchini, awe amekata leseni ya kusafirisha mazao nje ya nchi, awe na namba ya utambulisho ya mlipakodi (TIN) na awe na leseni ya biashara," alisema Bashe.
Jambo lingine alisema wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi na kuingia nchini kwenda kununua mazao na kuyasafirisha kwa leseni za biashara za madalali wa Tanzania, wamepigwa marufuku pia.
Bashe alisema utaratibu huo unalenga kuongeza eneo la ukusanyaji wa kodi na kuhakikisha wanawarasimisha wauzaji wa nafaka nje. “Tunataka wasafirishaji wa mazao nje waanze kupokea malipo kwa njia ya benki, haiwezekani tuuze mahindi moja ya nchi jirani tani 400,000 zaidi ya Sh300 bilioni halafu haionekani kwenye mfumo wa benki.
Yaliyotokea mikoani
Juzi, malori zaidi ya 120 yenye shehena ya mahindi kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyokuwa yakisafiri kwenda nje ya nchi yalizuiliwa kwa siku nne eneo la Njiapanda ya Himo mkoani Kilimanjaro yasiendelee na safari.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliwaamuru madereva kugeuza magari na kwenda kuyauza mahindi hayo katika masoko yaliyopo ndani ya nchi au kupeleka kwenye Ghala la Taifa mkoani Arusha na kwamba, atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria.
Babu alitoa maelekezo baada ya magari hayo yenye shehena ya mahindi kudaiwa kuvusha kinyemela na kwenda kuyauza nchi jirani ya Kenya. Hata hivyo, Bashe akilizungumzia hilo, alisema wafanyabiashara wengi hawakuwa na nyaraka sahihi ikiwemo leseni ya biashara na ya kusafirisha nafaka nje.