Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yazuia uuzwaji mifugo

Mifugo Pic Data Mahakama yazuia uuzwaji mifugo

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa amri ya kuzuia kuuzwa mifugo 1,448 wakiwamo ng’ombe 485 waliokamatwa wilayani Siha kwa kula mazao ya wakulima na kuwasababisha hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Mifugo hiyo wakiwamo ng’ombe hao 485 na kondoo na mbuzi wanaofikia 963, walikuwa wauzwe kwa mnada wa hadhara leo kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Siha, iliyotolewa Julai 12, 2022 na Hakimu Mkazi, Jasmin Abdul.

Hata hivyo, Julai 18, 2022, wafugaji wawili, Sinjore Laizer na Isaya Mollel walifungua maombi ya jinai namba 1 ya 2022 mbele ya Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi wakiomba mapitio ya uamuzi huo.

Wafugaji hao wamefungua maombi hayo dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na Newton Mwakale ambaye ni dalali wa mahakama na Jaji Semfukwe amepanga kesi hiyo kutajwa leo na wajibu maombi wote wajulishwe.

Mbali na amri hiyo, Jaji Simfukwe ameagiza mifugo hiyo isiuzwe hadi pale mahakama itakaposikiliza maombi hayo na kutoyatolea uamuzi. Makwale alilithibitishia gazeti hili jana kupokea amri hiyo ya zuio la Mahakama Kuu.

Advertisement Maombi ya DPP yalivyokuwa

Baada ya kukamatwa kwa mifugo hiyo, DPP akiwakilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Kassim Nassir akisaidiwa na mwendesha mashtaka, David Chishimba walifungua maombi ya jinai namba 17 ya mwaka 2022 wakiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa, kuzuiwa na kutaifishwa kwa mifugo hiyo.

Pia waliomba mahakama iteue dalali wa kuuza kwa mnada wa dharura mifugo hiyo na kwamba fedha zitakazotokana na mauzo hayo ziingizwe kwenye akaunti yenye jina la DPP iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akiwasilisha hoja za maombi hayo, wakili Nassir alisema mifugo hiyo iliingizwa kwa jinai kwenye mashamba ya wakulima wa Kijiji cha Olmolog na pia ilikiuka sheria ya udhibiti magonjwa wa wanyama.

Alisema mifugo hiyo inatoka nje ya Wilaya ya Siha na Mkoa wa Kilimanjaro na iliingizwa bila vibali vya maofisa mifugo kwa mujibu wa sheria ya magonjwa ya mifugo ya mwaka 2003.

Alisema mifugo hiyo lilishwa kwenye mashamba ya wakulima yenye mazao aina ya njegere, ngano, mbaazi na mazao mengine na hadi anawasilisha maombi hayo, hakuna aliyejitokeza na kudai mifugo yake.

Wakili Nassir aliiambia mahakama kuwa mifugo hiyo ilikuwa inahifadhiwa kwenye shamba la Ranchi ya Taifa (Narco) wilayani Siha ambalo halina miundombinu ya kutosha na wafanyakazi na inaweza kufa kwa kukosa huduma endelevu.

“Waathirika (wakulima) ambao mazao yao yaliharibiwa wanategemea kuuzwa kwa mifugo hiyo, ili wafidiwe hasara waliyoipata,” alieleza wakili huyo.

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Jasmin alisema alifika eneo inapotunzwa mifugo hiyo na kushuhudia yale aliyoyasema wakili Nassir na kuongeza kuwa ameshuhudia eneo hilo linakabiliwa na ukame.

Hakimu huyo alisema ukame huo unaweza kusababisha ng’ombe kufa kama hatua za haraka hazitachukuliwa. Kwa mujibu wa hakimu huyo, hadi anapoandika uamuzi huo Julai 12, hakuna mtu aliyekuwa amejitokeza kudai kuwa ni mmiliki halali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live