Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Kuu imelikataa tena pingamizi la "Tozo za Miamala"

TOZO Mahakama yaitupilia mbali kesi ya kupinga Tozo

Thu, 9 Sep 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu imetupilia mbali pingamizi la awali Serikali dhidi ya maombi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya kibali cha kufungua shauri la kupinga tozo kwenye miamala ya simu.

Hata hivyo, wakati mahakama hiyo ikitupa pingamizi la Serikali, pia imeyatupa maombi kama hayo yaliyofunguliwa na Mwanaharakati Odero Charles Odero baada ya kukubaliana na hoja moja ya pingamizi la Serikali kuwa hati ya kiapo chake kilichokuwa kinaunga mkono maombi hayo ina kasoro za kisheria.

Uamuzi huo wa umetolewa Jumatano Septemba 8,2021 na Jaji John Mgetta.

Akitoa uamuzi wa pingamizi la Serikali, Jaji Mgetta ametupilia mbali hoja zote tatu za Serikali akisema kuwa hazina mashiko.

Kuhusu hoja ya kwamba kanuni hizo haziwezi kupingwa kwa kuwa si uamuzi, hatia wala amri bali Serikali imetekeleza majukumu yake ya kisheria, Jaji Mgetta amekubaliana na hoja za mwombaji kuwa kanuni hizo zinaweza kupingwa.

Amesema kuwa utendaji au maamuzi yote yanayofanywa na maafisa wa Serikali kwa kuwa hii ni nchi ya Kidemokrasia lazima yaweze kudhibitiwa na Mahakama.

Kuhusu hoja ya kwamba shauri hilo lilifunguliwa bila kuwepo kwa maazimio ya bodi ya taasisi hiyo na kwamba mlalamikaji hakuonesha namna gani ameathirika au haki zake zimekiukwa, Jaji Mgetta amesema kuwa hoja hizo hazikidhi kuwa mapingamizi kwa kuwa si hoja za kisheria bali zinahitaji ushahidi.

Kwa uamuzi huo Jaji Mgetta ameamuru kuendelea na usikilizwaji wa maombi hayo ya kibali Septemba 20, 2021.

Kuhusu maombi ya Odero, Jaji ametupilia mbali hoja mbili kati ya tatu za pingamizi la Serikali lakini akakubaliana na hoja moja kuwa hati ya kiapo ina kasoro za kisheria kwa kuwa kuna aya ambazo zina hoja za hitimisho na nyingine maoni.

Hivyo amezifuta aya hizo zenye dosari na akasema kuwa baada ya kuzifuta aya hizo, zilizobaki kwenye kiapo hicho haziwezi kusimama zenyewe.

“Kwa sababu hizo nilizozitoa, kiapo hiki hakina nguvu na matokeo yake ninakitupilia mbali.”, amesema Jaji Mgetta.

Hata hivyo nje ya mahakama wakili wa Odero, John Seka amesema kuwa wanakwenda kufanya marekebisho ya kasoro hizo zilizobainishwa na mahakama na kwamba watarejea tena mahakamani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live