Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli atangaza neema kwa wakulima wa korosho

50259 Pic+korosho

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza Sh50 bilioni ziendelee kutolewa kwa wakulima wa korosho mkoani Mtwara.

Ametoa agizo hilo jana alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.

“Wananchi 18,000 wakiwamo wa kangomba watalipwa fedha zao lakini wawe kweli na korosho. Ukiwa huna korosho halafu ukasema unazo unatafuta kifungo. Wakati natoka Dar es Salaam leo, nimeagiza Sh50 bilioni ziletwe,” alisema.

Awali, Serikali ilisema malipo yote ya wakulima wa korosho mwaka huu yangekuwa yamekamilika Machi 31 lakini jana, Rais alisema ameagiza watu waendelee kulipwa. Tayari Sh578.7 bilioni kati ya Sh723.5 bilioni zinazohitajika zimeshalipwa.

Wakati wakulima wakilipwa kiasi hicho, Rais alifafanua malipo mengine yaliyofanywa kuwa ni Sh5.1 bilioni za usafiri na Sh6.4 bilioni zikitumika kununulia magunia. Pia, vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vimelipwa Sh3 bilioni wakati vyama vikuu vikilipwa Sh970 milioni na wasimamizi wa maghala Sh6.6 bilioni pamoja na Sh1.3 bilioni zilizolipwa kwa mratibu.

“Wote wenye madai halali watapata fedha zao, nimeshaagiza watu waendelee kulipwa lakini wasitaje majina ya watu wengine wala vyama vya ushirika visiandikishe majina hewa. Mtwara tumeelewana… Mtwara kuchelee!” alisema Rais Magufuli.

Related Content

Ahadi ya Rais ni muendelezo wa utekelezaji wa uamuzi alioufanya Novemba mwaka jana alipotangaza kwamba Serikali itanunua korosho yote kwa Sh3,300 kwa kila kilo moja baada ya wanunuzi binafsi kususa kununua kwa zaidi ya Sh1,700 kwa kilo na aliiagiza Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuanza ununuzi wa zao hilo muhimu kwa uchumi wa Taifa huku Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likipewa jukumu la kuzisafirisha.

Kufanikisha ununuzi huo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ilipewa jukumu la kutoa fedha.

Kwenye ununuzi, Serikali ilitangaza kufanya uhakiki kwa lengo la kuondoa walanguzi ikitaka wauzzaji wawe wakulima wenyewe ili kuwaongezea tija.

Kuwatoa shaka wote wanaosubiri malipo yao, jana Rais alisema Serikali haikuzichukua korosho hizo ili kufanya biashara, bali kuwaepusha na bei ndogo iliyotangazwa na Bodi ya Korosho Tanzania iliyopendekeza kilo moja iuzwe kwa Sh1,500 ingawa baadaye ilipanda hadi Sh2,100

“Tumeanza kubangua tani 15,000. Niwaombe Watanzania wenzangu na wana Mtwara, umefika wakati sasa wa kuwa na viwanda vya ubanguaji korosho,” alisema.

Mkuu wa Mkoa Mtwara

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema ameagiza ofisi za wakuu wa wilaya za mkoa huo kuanza kupokea malalamiko ya wakulima katika makundi maalumu kuhusu ununuzi wa zao hilo, kubwa ikiwa ni baadhi ya majina ya akaunti kutofautiana na majina ya wakulima.

“Kuna Sh10 bilioni hazijapelekwa katika akaunti kwa sababu ya utofauti huo, lakini baadhi ya wakulima wamelalamika kutolipwa malipo yao kutokana na ubadhirifu wa viongozi wa vyama vya msingi kwenye maeneo yao na wakulima kubakia na vyeti vyao, mfano Chama cha Msingi Newala kilipokea tani 12, zikakosa ubora kwenye maghala makuu, badala ya kurudisha kwa wakulima wakamtafuta mtunza ghala wanayemfahamu na kumuuzia korosho hizo,”

Mkulima wa korosho kutoka Tunduru, Ruvuma, Sadick Said alisema ni jambo la heri kuendelea na malipo hayo kwani shughuli nyingi za kilimo zilikuwa zimeanza kukwama.

“Ni wajibu wa Serikali kulipa madeni hayo na tunavyoongea hivi sasa hali siyo nzuri, shughuli zimesimama za kilimo kwani tunategemea fedha hizo, kwa hiyo tunashukuru kwa uamuzi huo,” alisema Said.



Chanzo: mwananchi.co.tz