Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli: Tutanunua korosho kwa Sh3,300 kwa kilo

26832 Pic+magu TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali itanunua korosho zote za wakulima zilizolimwa mwaka huu 2018 na itachukua dhamana ya kuzitafutia soko.

Korosho hizo zitanunuliwa kwa bei ya Sh3,300 malipo ambayo yatafanywa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri na manaibu waziri walioteuliwa Jumamosi iliyopita ya Novemba 10, 2018.

Amesema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndiyo watakuwa na jukumu la kusimamia kuhakikisha ulinzi kwenye maghala, korosho zinapimwa na wakulima wanalipwa.

Pia, ameelekeza vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupewa kazi ya kubangua korosho.

“Korosho zote tunanunua na tukipata hasara potelea mbali, Serikali haipatagi hasara, serikali ni mali ya wananchi.”

“Hatuwezi kuendelea kuwadhulumu wananchi wetu, CDF (Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi- Jenerali Venance Mabeyo) panga kikosi chako vizuri kila ghala lilindwe na jeshi, korosho ipimwe na wakulima walipwe fedha zao zote, asitokee mtu wa kusema alikuwa anamdai mkulima,” amesema Rais Magufuli.

“Jeshi likishapokea hizo korosho wanajeshi watazipeleka kwenye maghala makubwa na nimeambiwa wameshatawanywa tayari kwa kazi hiyo,” amesema.

Amesema baadhi ya tani za korosho zitakazonunuliwa zitapelekwa kwenye kiwanda cha Buko kilichopo Lindi kwa ajili ya kubanguliwa.

Kiwanda hicho ambacho kimerudi mikononi mwa Serikali baada ya mwekezaji kushindwa kukiendeleza, Rais Magufuli amekikabidhi rasmi kwa jeshi kuanzia leo Jumatatu.



Chanzo: mwananchi.co.tz