Serikali imeandaa dira ya mwaka 2030 inayokusudia kuwekeza katika tafiti za ukusanyaji taarifa za viashiria vya madini mbalimbali nchini, hatua itakayochochea mageuzi katika maeneo sita, ikiwamo uhakika wa kupata madini na mikopo ya uwekezaji kutoka taasisi za kifedha.
Maeneo mengine ni kuwezesha upatikanaji wa data za miamba yenye malighafi ya mbolea, data za miamba yenye maji kwa ajili ya sekta ya umwagiliaji na vyanzo vya maji ya kisima katika maeneo yenye changamoto nchini pamoja na utambuzi wa maeneo yenye ardhi kwa mahitaji mbalimbali.
Kwa mujibu Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), tafiti za kina za jiofizikia ambazo hutumia usafiri wa anga kukusanya data kwa njia ya kupiga picha angani kwa ajili ya uchunguzi wa awali zimefanyika kwa asilimia 16 pekee kati ya vitalu 322 vilivyogawanywa katika ardhi ya Tanzania. Kila kitalu kina ukubwa wa kilomita za mraba 2,916.
Jana, Serikali ilisema eneo hilo la asilimia 16 limewezesha sekta hiyo kufikia mchango wa asilimia 9.1 ya Pato la Taifa (GDP), asilimia 15 ya mapato ya ndani, Dola bilioni 3.3 ya mauzo ya nje, mchango wa asilimia 56 ya fedha za kigeni na Dola milioni 50 kwa huduma na manunuzi ya ndani mwaka 2022/23.
Kutokana na mwenendo huo, dira hiyo isemayo “Madini ni maisha na utajiri” inakusudia kutekelezwa chini ya GST ili kuongeza akiba ya maeneo yenye viashiria vya madini kwa asilimia 50 kwa miaka sita iliyobakia kwa bajeti ambayo haikuwekwa wazi na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Mavunde alitoa mwelekeo huo jana, alipofungua mkutano wa kwanza kati ya sekta ya madini na sekta ya fedha uliokusudia kutafuta mwarobaini wa changamoto za mikopo.
“Bila taarifa za miamba, hata utoaji wa leseni utaonekana ni makaratasi tu. Huwezi kujua madini yako ndio sababu kubwa ya kukosa mikopo kwenye taasisi za fedha, kwa hiyo tumepanga hadi 2030 tuwe na asilimia angalau 50 ya data za miamba yote nchini kutoka asilimia 16 ya sasa.
Mavunde alitaja manufaa mengine ya dira hiyo ni kuvuna maji kwa ajili ya mabwawa ya kuhifadhi lita bilioni 900 za umwagiliaji na ushawishi wa uwekezaji mkubwa.
Pia kuchochea uwekezaji wa viwanda vya mbolea kupitia miamba yenye malighafi ya mbolea, hivyo kuepuka uagizaji wa tani 350,000 kila mwaka na kupata mwarobaini wa changamoto ya hekta milioni 3.7 nchini zilizoathiriwa na madini ya chumvi.
Changamoto BoT
Mavunde alitoa rai ya kuepuka utoroshaji madini, huku akikiri changamoto za ununuzi wa madini chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Tuna mitambo sita ya uchenjuaji, lakini miwili ndiyo imethibitika kwa viwango vizuri, BoT inatakiwa kununua madini kwenye mitambo hii, lakini mzigo (madini) mwingi hauendi huko, wachimbaji wengi hupatiwa mikopo na wanunuzi wakati wa uchimbaji ili wawauzie wanapopata madini,” alisema.
Michael Muno, Meneja Msaidizi wa Masoko ya Nje ya Fedha wa BoT alisema benki hiyo iko tayari kuwezesha wachimbaji wadogo. “BoT iko tayari kuwezesha hilo kupitia mikopo itakayotolewa na taasisi nyingine za kifedha, tutakaa na Stamico kuweka utaratibu wa kufanya hatua hiyo,” alisema.
Hoja za wachimbaji
Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wadogo Tanzania (Femata), John Bina alishauri Serikali kuingilia kati anguko la uzalishaji wa madini ya Tanzanite na uwezeshaji wa BoT kwa wachimbaji ili kukusanya akiba nyingi ya madini.
Pia alishauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wanaoingiza madini nchini kwa ajili ya kuchenjua katika mitambo ya ndani, ili kuvutia wengi na kuanzisha mikakati ya kuwa kituo kikubwa cha biashara ya madini Afrika pamoja na kasi ya uwekezaji wa makaa ya mawe.
Wakati Bina akishauri hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Venance Mwasse alitaja changamoto namna wanavyozishughulikia kwa wachimbaji wadogo ambazo ni masoko, mitaji, data za miamba, elimu matumizi ya teknolojia na mikopo.
“Tayari tumeshaanza kutafuta suluhisho, tumeagiza mashine 15 za kuchimbia, tayari tano zimefika. Tuna kampeni ya elimu nchi nzima,” alisema Mwasse.
Mikopo bado ngumu
Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi alitaja kuwa inayokwamisha mikopo kwa wachimbaji wadogo ni ukosefu wa data za mashapo (miamba yenye madini).
Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto hizo, taasisi za kifedha bado zinatoa mikopo kwa baadhi ya wadau wa sekta hiyo, wakiwamo wasambazaji wa bidhaa na huduma kwa maombi ya kawaida.