Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mageuzi makubwa yafanywa Bandari za Ziwa Tanganyika

D0bf9887e15053d046494308a3f0d489.PNG Ufanisi unatajwa kuongezeka

Tue, 29 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, eneo aliloupiga mwingi kiutendaji ni pamoja na maboresho makubwa ya bandari nchini zikiwemo sita zilizopo katika Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika lina bandari 19 ndogo na kubwa.

Kati ya hizo, ukiacha Kigoma, sita zinaendelea kufanyiwa maboresho makubwa ambazo ni Karema, Kibirizi, Kasanga, Kabwe, Kipili, Karemo na Kagunga. Kigoma yenyewe ina mradi mkubwa wa tofauti lakini kwa mwaka mmoja imewezeshwa pia kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika.

Uongozi wa Bandari za Ziwa Tanganyika zilizo chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) unamshukuru Rais Samia kwa maboresho hayo makubwa yanayofanywa na serikali yake ili kuziwezesha bandari hizo kutoa huduma kwa viwango vya kimataifa. Kwa bandari zote za Ziwa Tanganyika, maboresho yaliyofanywa yamewezesha kusafirisha shehena ya tani 282,221, sawa na ongezeko la asilimia 19 ya lengo la kusafirisha tani 237,806 kwa kipindi cha kati ya Machi 2021 hadi Februari mwaka huu (2022).

Hata hivyo, uwezo wa bandari hizo kwa sasa ni kusafirisha takribani tani 800,000, hivyo maboresho hayo yakikamilika uwezo utaongezeka.

Pamoja na kwamba Bandari ya Kigoma inasubiri maboresho makubwa, eneo mojawapo la maboresho yanayoanza kuleta tija ni kuwezeshwa mradi wenye maeneo matatu ambayo ni ujenzi wa Ofisi ya Meneja wa Bandari, jeti ya Ujiji na gati ya bandari ndogo ya Kibirizi.

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Manga Gassaya, akizungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) juzi katika ofisi za TPA, Kigoma, alisema Rais Samia katika kipindi cha mwaka mmoja, amewafanyia makubwa ikiwemo kuwapa fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari za ziwa hilo.

Katika mradi huo wa Kigoma, serikali ilitoa Sh bilioni 32.5 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi iliyokamilika kwa asilimia 100 na inasubiri kufunguliwa muda wowote kuanzia sasa, jeti ya Ujiji na gati ya bandari ndogo ya Kibirizi ambayo iko umbali wa kilometa moja kutoka Bandari ya Kigoma. Akifafanua zaidi, Gassaya anasema, jeti ya Ujiji maboresho yamefikia asilimia 35 na gati ya Kibirizi imefikia asilimia 70.

Akieleza kuhusu uboreshaji wa jumla wa bandari hizo mbali na bandari ya Kigoma, Gassaya anasema utakamilika Juni mwaka huu na huduma zitazidi kuboreka.

“Niwahakikishie wateja wetu kuwa huduma zitaboreka zaidi kutoka kukaa mizigo bandarini kwa karibu mwezi na kuwa ndani ya wiki na hii imeshaanza hata kabla ya Juni, huduma zitakuwa kwa viwango vya kimataifa. Hii yote ni kazi nzuri ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan,” anasema Gassaya.

Sambamba na hilo anasema zipo hekta 67 za bandari kavu mkoani Kigoma na kwamba eneo hilo litaboreshwa ili kupokea kontena nyingi zaidi zinazotarajiwa kutumia bandari hizo. Gassaya anasema nchi zinazotumia zaidi bandari hizo na asilimia ya mizigo inayosafirisha kwenye mabano ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (76), Burundi (15) na Zambia asilimia 0.1.

“Bandari za Tanzania zinakuwa chaguo namba moja la watumiaji Kusini mwa Afrika kwani waliokimbia kwa sababu mbalimbali, wanarudi hasa kwa kuwa huduma zinatolewa kwa haraka na kwa ufanisi, usalama na ulinzi mkubwa,” anasema Gassaya. Gassaya anasema hivi sasa wateja wanaotumia bandari hizo wanapata huduma ndani ya wiki tofauti na awali iliweza kuchukua mwezi.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa TPA, makao makuu, Nicodemus Mushi, anasema uboreshaji huo ni kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia katika kuwekeza kwenye vifaa ambapo alitoa zaidi ya Sh bilioni 500 kwa maboresho ya bandari zote nchini katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Ni vyema watu wakajua kuwa, ongezeko la meli za mizigo zinazosubiri kuingia bandarini hasa Dar es Salaam, ni neema na si laana,” anasema Mushi.

Mushi anasema nguvu kubwa ya maboresho imewekwa katika Bandari ya Dar es Salaam kama bandari mama lakini fedha hizo zinaboresha bandari zote zilizo chini ya TPA nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live