Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuta na gesi vyazua balaa COP28

Mafuta Na Gesi Mafuta na gesi vyazua balaa COP28

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku 13 za majadiliano ya mwelekeo wa dunia kwenye ya mabadiliko ya tabianchi zimekwisha jana huku zikiacha mvutano mzito juu ya uondoshwaji au kubakiza matumizi ya gesi, mafuta na makaa ya mawe kwa nchi mbalimbali duniani.

Hayo yamejitokeza kwenye majadiliano ya wadau wa mazingira duniani waliokutana Dubai kwenye mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC-COP28).

Licha ya nchi hizo kujadili mustakabali kwenye sekta za kilimo, nishati, fedha na mengine, kubwa ilikuwa ni upatikanaji wa rasimu ya kwanza ya maandishi ya ajenda (GST) chini ya makubaliano ya Paris, COP21 ya mwaka 2015).

GST ni mchakato chini ya UNFCCC, unaotathmini maendeleo ya pamoja ya nchi katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.

Katika mchakato huo, vipo vipengele saba vinavyofuatiliwa ambavyo ni tathmini ya jitihada za hiari zilizowekwa na nchi kwenye kukabili mabadilko ya tabianchi (NDC), fedha za kukabiliana nayo, teknolijia na uwezo wa nchi, njia za kukabiliana, madhara na uharibifu, uwazi na mwenendo wa uzalishaji wa hewa joto.

Kati ya hayo, jambo lililozua mjadala kwenye rasimu hiyo ni mwenendo wa uzalishaji wa hewa joto (kaboni, methane) zinazotokana na matumizi ya nishati chafu za mafuta, gesi na makaa ya mawe.

Kwenye rasimu hiyo yenye kurasa 21 na vipengele 283, kipengele cha 39 chenye vifungu vinane kinazungumzia nishati hizo. Mwanzo kinanukuu, “... tunatambua hitaji la upunguzaji wa kiwango kikubwa, na haraka uzalishaji wa hewa chafu na kutoa wito kwa wanachama kuchukua hatua”.

Kipengele kimojawapo kinapendekeza, “kupunguza matumizi na uzalishaji wa nishati chafu, kwa utaratibu wa haki na usawa ili kufikia uzalishaji sifuri ifikapo, kabla, au karibu na 2050”.

Pia, malengo mengine ni kuanzia sasa, kupunguza matumizi ili kuendelea kudhibiti halijoto chini ya sentigrade 1.5 hadi ifikapo mwaka 2030.

Suala hilo liliwaibua wanaharakati walioshiriki mkutano huo wakihitaji dunia ikubaliane kuachana na matumizi ya nishati chafu kwa mazingira ya sasa badala ya kusubiri miaka mingi ijayo.

Hata hivyo, wachambuzi waliozungumizia jambo hilo, walipishana kauli juu ya nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, juu ya utayari wa utekelezaji wa jambo hilo.

"Kuondoa nishati kisukuku (nishati chafu) kutachukua muda sana. Kwa mfano, kubadilisha magari kutoka kwa kutumia mafuta hadi nishati safi, bado tuko nyuma sana,” amesema.

Profesa Eliakimu Zahabu, kiongozi wa timu ya Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC).

Profesa Zahabu amesema mabadiliko mazuri yanaweza kutokea ikiwa nchi zenye nguvu zitaongoza kwa mfano na kutoa muda kwa nchi zinazoendelea kubadilika taratibu ili mabadiliko hayo yasiathri uchumi.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uagizaji wa mafuta kwa mwaka 2022 ulikuwa zaidi ya Sh7 trilioni, na kufanya kuwa bidhaa iliyochukua fedha nyingi zaidi za kigeni.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Power Shift Africa, Mohamed Adow alisema Afrika inaweza kuachana na nishati hizo lakini haihitaji msukumo huo, kwani utafiti unaonyesha uchangiaji wake katika uchafuzi wa mazingira ni chini ya asilimia nne ukilinganisha na nchi zilizoendelea.

“Afrika haitakiwi kuwa na msukukumo kwani kuanzia mwanzo haina uhitaji mkubwa wa kupunguza matumizi ya nishati chafu kwani haizalishi wa kiwango kikubwa. Wao ndio waache uzalishaji,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema nchi nyingi zilizoendelea zilitumia nishati hizo kunufaika na waliochelewa kufikia hatua hii, wanakatishwa tamaa na kuwekewa vikwazo kujihusisha na shughuli hizo, jambo linalizuia maendeleo kwao.

"Nishati hizi bado ni rasilimali ya bei nafuu na inayotegemewa na nchi nyingi zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na Tanzania, nchi hizo zikiiacha zitapata hasara kubwa kutokana na ajenda hiyo," amesema.

Mgaya alisema nchi zenye uchumi mkubwa ikiwamo Marekani, China, Uingereza na Russia zinaendelea kuwa miongoni mwa wachafuzi wakubwa zaidi duniani.

Takwimu za mtandao wa The Union of Concerned Scientists (UCS) za mwaka 2020 zinaonyesha China inaongoza kwa kuzalisha hewa chafu kwa aslimia 31 ikifuatiwa na Marekani asilimia 13, India asilimia 7, Russia asilimia 3 na nyingine.

Kuhusu suluhisho, Adow alisema suluhu kwa haya ni matumizi ya nishati jadidifu.

“Tafiti zinaonyesha Bara la Afrika lina vyanzo vyenye uwezo wa kuzalisha nishati safi ya vyanzo jadidifu kwa mara 50 zaidi ya mahitaji ya dunia itakapofika 2050. Kinachohitajika ni mikakati,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live