Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuta, dhahabu zilivyookoa uchumi

0f7b3cc91b8570edc928a7a66296fa0e Mafuta, dhahabu zilivyookoa uchumi

Wed, 10 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Fedha na Mipango imetaja sababu za mwenendo wa uchumi wa Tanzania kuendelea kuimarika wakati dunia ikipambana na Covid-19, kuwa ni baada ya kupata unafuu kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta na kuongezeka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia.

Pamoja na hayo, imebainisha sababu nyingine kuwa ni maono na ujasiri wa Rais John Magufuli ya kuruhusu shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea wakati wa mlipuko huo.

Hayo yamebainishwa bungeni juzi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, wakati akiwasilisha taarifa za Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/22. Dk Mwigulu alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka jana, uchumi ulikua kwa asilimia 4.7.

Alitaja sekta zilizokua kwa kasi zaidi kuwa ni ujenzi (asilimia 13.6), uchimbaji madini (9.9%); habari na mawasiliano (9.0%); uchukuzi na uhifadhi wa mizigo (8.9%); na shughuli za kiufundi, kitaalamu, na kisayansi (8.8%).

Alisema kasi hiyo ya ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 6.9 kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 imewezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati cha chini kutoka kundi la nchi za kipato cha chini.

“Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya Julai 2020, wastani wa pato la mtu mmoja mmoja uliongezeka kutoka shilingi 1,990,462 (sawa na dola za Marekani 980) mwaka 2015 hadi shilingi 2,577,967 (sawa na dola za Marekani 1,080) mwaka 2019, hivyo kuvuka kigezo cha dola za Marekani 1,036 cha kuingia katika kundi la nchi za kipato cha kati cha chini,” alifafanua waziri huyo.

Aidha, alisema utegemezi wa kibajeti umepungua kutoka asilimia 14.0 ya bajeti halisi mwaka 2014/15 hadi asilimia 9.3 mwaka 2019/20. Alisema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kufikia lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati cha chini mapema zaidi ikilinganishwa na matarajio yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Alisema pia Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 23 za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, zenye uchumi wa kipato cha kati cha chini. Na katika nchi 16 za SADC, Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zilizo na uchumi wa kipato cha kati cha chini.

“Tanzania na Kenya ndiyo nchi pekee zenye uchumi wa kipato cha kati cha chini katika nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi na utekelezaji madhubuti wa sera na mipango ya maendeleo na kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji huduma kwa wananchi kama vile elimu, afya, maji, umeme na miundombinu.

Alisema maboresho yaliyofanyika katika huduma hizo yamepunguza umasikini na kuboresha maisha ya wananchi, mathalani umaskini wa mahitaji muhimu umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18.

Aidha, alisema umasikini usio wa kipato umekuwa na mabadiliko chanya ambapo idadi ya watanzania wenye bima ya afya imeongezeka kutoka asilimia 27 mwaka 2016/17 hadi asilimia 34 mwaka 2018/19; idadi ya vifo wakati wa kujifungua imepungua kutoka 432 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi 321 mwaka 2019/20.

Alisema pia idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano imepungua hadi 50 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2019/20 kutoka vifo 67 mwaka 2014/15; vifo vya watoto wachanga vimepungua hadi 36 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2019/20 kutoka vifo 43 mwaka 2015/16.

Alisema kiwango cha ufaulu mitihani ya darasa la saba pamoja na sekondari (Kidato cha nne) kimeongezeka kutoka asilimia 67 na asilimia 68 mwaka 2015 hadi asilimia 81.5 na asilimia 80.7 mwaka 2019 mtawalia.

“Idadi ya wanufaika wa mkopo wa elimu ya juu imeongezeka kutoka wanufaika 125,126 mwaka 2015 hadi 145,000 mwaka 2020; hali ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini imeongezeka kufikia asilimia 84 na asilimia 70.1 mwaka 2019 kutoka asilimia 74 na asilimia 47 mwaka 2015 mtawalia,” alieleza.

Chanzo: habarileo.co.tz