Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru amesema tija ikiongezeka katika uzalishaji wa bidhaa zinazotegemewa na Watanzania, nchini utasaidia kuondokana mfumuko wa bei.
Mafuru amesema hayo jana Jumatano Februari 8, 2023 katika mjadala kwa njia ya Twitter (Twitter Space) ulioratibiwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, uliohusu 'Serikali imechukua hatua kukabiliana na mfumuko wa bei, nini maoni yako'.
Mjadala huo umeshirikisha watu mbalimbali wakiwemo wakulima, wanasiasa na viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri, Dk Mwigulu Nchemba wa Fedha na Mipango pamoja na Hussein Bashe wa Kilimo.
Hata hivyo, Mafuru amesema tatizo la mfumuko wa bei ni la kudumu la uchumi wowote duniani, akisema Serikali za mataifa mbalimbali bado zinaangika katika kukabiliana nalo.
“Kuwepo kwa sekta mbalimbali zitakazozalisha bidhaa kwa wingi nchini ili kuondokana na kuagiza na kununua nje, hata mataifa mengine yatakuja kununua kwetu.
“Tuendelea kuwavutia wawekezaji ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi, mfano hivi sasa uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye uzalishaji wa sukari na baada ya miaka miwili tutaacha kabisa kuingiza sukari na tutakuwa wasambazaji kwa nchi jirani,” amesema Mafuru.
Akichangia mjadala huo, Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi wa ACT-Wazalendo, Emmanuel Mvula amesema pamoja na Serikali kuanisha hatua mbalimbali za kukabiliana na mfumuko wa bei za bidhaa lakini bado njia hizo hazijasaidia kwa sababu hazijatekelezwa kwa ufanisi.
Mvula amesema bajeti ya kilimo imeongezeka tofauti na miaka iliyopita, akisema hatua hiyo ililenga kuboresha uzalishaji wa chakula ili kudhibiti mfumuko wa bei. Lakini tangu bajeti hiyo ipitishwe fedha zilizotolewa ni chache,
“Sasa hivi msimu wa kilimo upo ukingoni, hatua hizi ni maneno zaidi sio vitendo haziwezi kukidhi. Serikali imejikita kutoa mbolea ya ruzuku, lakini kumekuwa na malalamiko kwanza haiwafiki wananchi kwa wakati, tena wale wananchi wa vijijini wanajikuta wakiipata kwa gharama kubwa.
“Mfumo wa mbolea ya ruzuku inazuia hata wale wenye uwezo kushindwa kununua kutokana na mfumo huu,” amesema Mvula.