Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maelfu wajiandikisha kushiriki mkutano wa chakula Tanzania

Vyakulaaaaa Maelfu wajiandikisha kushiriki mkutano wa chakula Tanzania

Wed, 30 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Watu 3,300 wamejiandikisha kushiriki mkutano wa kimataifa wa kilimo unaotarajiwa kufanyika nchini Septemba 5 - 8 mwaka huku ukilenga kuangazia mifumo ya chakula Afrika.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi mwishoni mwa wiki hii hadi kufikia watu 4,000, idadi ambayo ni mara mbili ya ile ya mwaka jana wakati wa mkutano huo uliofanyika Rwanda ukihudhuriwa na watu 2,000.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 30, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa majadiliano kuhusu ufadhili wa kilimo, fursa na changamoto zake nchini Tanzania.

Akifungua majadiliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri amesema Tanzania ilishinda kuandaa mkutano huo kutokana na sababu mbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la bajeti katika kilimo, utafiti, mbegu na kushirikisha vijana na wanawake kwenye kilimo.

“Tulishinda kwa sababu nyingi, kwanza ni utayari wa nchi kuendesha ajenda ya chakula kwa ajili ya dunia. Nchi nyingi zinasema zinataka kubadilisha hali ya kilimo, zinataka kubadilisha hali ya chakula lakini nani amefanya hivyo, sisi tayari tumeanza kufanya hivyo,” amesema.

Amesema Tanzania ilishinda kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa sababu ya kuongezeka kwa bajeti ya kilimo ambayo imepanda kutoka Sh298 bilioni hadi Sh970 bilioni katika bajeti ya mwaka 2023/24.

Amesema bajeti hiyo imeelekezwa kwenye maeneo makubwa manne, ambayo ni umwagiliaji. Amesema Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini umwagiliaji unafanyika kwenye hekta 700,000, sawa na asilimia 10.

“Malengo yetu kufikia mwaka 2030, angalau asilimia isiyopungua 25 au 30 ya ardhi yetu iwe kwenye umwagiliaji. Kitendo hiki kilionyesha utayari wetu wa kuendesha ajenda ya chakula,” amesema.

Mambo mengine ni pamoja na utafiti ambayo bajeti yake imeongezeka kutoka Sh11 bilioni mwaka 2021 hadi Sh45 bilioni, amesisitiza kwamba bajeti hiyo imekuwa ikitoka. Mengine ni bajeti ya mbegu na ushirikishaji wa vijana na wanawake katika kilimo.

Kwa upande wake, mshauri wa kilimo katika benki ya NMB, Isaac Msasu, amesema benki yake imetoa mikopo ya Sh1.6 trilioni katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuifanya sekta hiyo inayochangia ajira kwa asilimia 66 kuchangia katika pato la Taifa.

“Tunatoa mikopo ya muda mrefu kwenye sekta za kilimo ufugaji na uvuvi na mikopo yetu ina riba ya asilimia tisa tu kwa mkulima mmoja mmoja,” amesema Msasu wakati akifafanua ushiriki wa benki.

Chanzo: Mwananchi