Wakati wafanyabiashara wa fedha za kigeni wakitaka kuhakikishiwa mazingira mazuri ya biashara, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imewataka kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria za nchi.
Hayo yamesemwa leo Agosti 16, 2023; katika mkutano wa wadau wa biashara ya fedha za kigeni, ulioandaliwa na BoT jijini hapa, huku Meneja Msaidizi Kitengo cha Fedha wa benki hiyo, Omari Msuya, akiitaja sheria hiyo na kanuni zake.
Msuya ameitaja sheria hiyo kuwa ni ile ya mwaka 1992, kifungu cha 5(a) na cha sita ambacho kinachoipa mamlaka BoT kusimamia na kuidhinisha biashara ya fedha za kigeni.
"Kifungu cha 7(a) cha sheria, Gavana anaweza kuweka kanuni na maelekezo na miongozo. Kwa sasa Gavana ameshaweka kanuni za usimamizi wa maduka ya kubadilisha fedha, kwa mujibu wa kifungu cha 5(a) na 7,” amesema.
Hivyo, ofisa huyo wa BoT amewahamasisha wafanyabiashara kujitokeza zaidi wakiwa na vigezo vikiwemo vya kuwa na mtaji wa Sh1 bilioni na hivyo kufanya biashara bila ya kuwa na wasiwasi.
“Hali ilivyo sasa hivi, kuna msukumo mkubwa wa watu kufungua maduka. Ila tunatahadharisha watu wasije kuingia mtego wa kufanya biashara hii bila ya kuwa na leseni,” amesema.
Akifunga mafunzo hayo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watashirikiana na BoT na wafanyabiashara hao kuhakikisha sheria zinafuatwa.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, litaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, kuhakikisha sheria za biashara za kigeni zinafuatwa. Elimu iwe endelevu,” amesema.
Awali baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, wameiomba Serikali kuwaondolea hofu ya kufungiwa maduka yao ili kukuza bishara hiyo.
Mwaka 2018 baadhi ya maduka ya fedha za kigeni mkoani Arusha yalifungwa kutokana na ukaguzi uliofanywa na vyombo vya dola vikishirikiana na maofisa wa Benki Kuu Tanzania (BoT), huku ikielezwa kuwa mengi ya maduka hayo yalikuwa na viashiria vya utakatishaji fedha.
Licha ya baadhi yao kuishukuru Serikali kwa kuonyesha ushirikiano uliorejesha imani yao katika biashara, mmoja wa wafanyabiashara hao Deogratius Marandu, amesema kutokana na matukio ya maduka hayo kufungwa, bado kuna hofu miongoni mwao.
“Tangu Serikali ilipofunga biashara, bado watu wana hofu, ni vizuri hata Polisi kututoa hofu. Hata Gavana alituita akatuambia tuko kwa ajili ya biashara na anapitia upya kanuni.
“Hata ukiangalia wafanyabiashara waliohudhuria hapa ni wachache sana, wangekuwepo hapa na kama anavyosisitiza Gavana wa Benki Kuu kwamba anataka aone biashara ikishamiri, kwa kushirikiana na Polisi biashara itaongezeka zaidi,” amesema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mohamed Ally alisema awali wafanyabiashara walikuwa na hofu lakini sasa BoT imewaondolea hofu hiyo.
“Awali mtu akiwa na fedha ya kigeni anakuwa na hofu kama ameshika bangi, lakini sasa tumeambiwa ni rahisi kufanya biashara,” amesema.