Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maduka ya dola bado yafungwa

28416 Maduka+pic TanzaniaWeb

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Maduka ya kubadilisha fedha katika jiji la Arusha jana yaliendelea kufungwa huku mabenki yakiendelea kubadilisha fedha hizo kwa masharti.

Maduka hayo, ambayo yamefungwa tangu Ijumaa katika operesheni iliyofanywa na Benki Kuu ya Tanzanian (BoT) kwa kushirikiana na vyombo vya dola, yamesababisha adha kwa wafanyabiashara sekta ya utalii, wafanyakazi na watalii.

Jiji la Arusha ni miongoni mwa maeneo nchini yanayoongoza kwa matumizi ya dola kutokana na utalii na uwepo wa taasisi nyingi za kimataifa.

Ismail Lenana ambaye anafanya kazi ya kubeba mizigo ya watalii alisema amepata shida kubadilisha fedha kutokana na masharti ya benki.

“Nimeenda benki wanaomba kitambulisho na kutakiwa kujaza fomu ndio ubadili fedha, naona kama ni usumbufu,” alisema.

Lenana alisema kwa kawaida wamekuwa wakilipwa kwa dola na watalii, walizoea kwenda kubadilisha fedha kwenye maduka bila taratibu za kujaza fomu wala kutoa vitambulisho.

Julius Peter, mkazi wa Sanawari aliomba Serikali kumaliza uchunguzi katika maduka ya fedha ili huduma irejeshwe.

“Shida ya benki kwanza tunanunua dola kwa gharama kubwa na kubadilisha shilingi ni kidogo” alisema.

Ofisa mmoja wa benki ya NMB tawi la Clock Tower, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake alikiri ongezeko la wateja wa kubadili fedha.

Alisema licha ya malalamiko ya wateja juu ya taratibu za kubadili fedha, wao wanafuata taratibu za benki kuu.

“Mtu mwenye dola kama anataka kubadilisha lazima awe na kitambulisho na kujaza fomu ya benki” alisema.

Alisema kwa upande wa watalii, wanalazimika kutoa nakala ya pasi ya kusafiria.

Hata hivyo, hadi jana hakuna ofisa wa BoT wala polisi ambao walikuwa tayari kuzungumza juu ya sakata la maduka hayo.

Mkurugenzi wa benki kuu tawi la Arusha, Charles Yamo alisema juzi kuwa operesheni ya maduka hayo ilifanywa na timu maalumu kutoka makao makuu.



Chanzo: mwananchi.co.tz