Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani wawaangukia wadau mfumo ukusanyaji mapato

Efd Machineee.jpeg Madiwani wawaangukia wadau mfumo ukusanyaji mapato

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani hapa, wamewaomba wadau kushirikiana ili kufanikisha kufungwa kwa mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato (GoTHOMIS) katika vituo vya afya 41 vya wilaya hiyo.

Wito huo ulitolewa jana na madiwani hao katika baraza maalum la kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Diwani wa Kata ya Baray, Elitumaini Magnus, alisisitiza kuwa ufungwaji wa mifumo hiyo utaongeza kasi ya ukusanyaji mapato.

"Kwa sasa halmashauri hii imefunga mfumo huo katika vituo vya afya saba tu, vituo 34 bado havijafungwa," alisema.

Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Karatu, Dk.Victor Kamazima alithibitisha vituo saba kufungwa mfumo huo na 34 havijafungwa.

"Mwaka huu wa fedha (2023/44) kabla haujaisha tumetenga shilingi milioni 34 kwa ajili ya kununua vifaa vya awali ikiwamo kompyuta ili tuanzie hapo," alisema.

Dk. Kamazima alisema kwa mwaka ujao wa fedha wa 2024/25, wametenga Sh. milioni 43 kwa ajili ya kufunga vifaa vya kisasa kwa vituo vilivyobaki.

Alisisitiza kuwa mchakato wa kufunga mfumo huo unaendelea kadri bajeti itakavyoruhusu kulingana na mapato wanaokusanya katika kila kituo cha afya.

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa, aliiagiza idara ya elimu msingi na sekondari kutoa uwiano sahihi wa idadi vitabu vya kiada na ziada ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi kujisomea.

Musa aliagiza hadi Septemba mwaka huu mfumo huo ufungwe ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.

Vilevile aliagiza madeni ya watumishi na wazabuni yalipwe ili kuondoa malalamiko kwa watoa huduma katika wilaya hiyo.

"Zingatieni utunzaji wa kumbukumbu za wadaiwa wenu maana kuna mahali ukifuatilia kumbukumbu za madeni wanayodai wazabuni mengine huyaoni, hivyo hakikisheni mnalipa mnayodaiwa," alisema.

Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Liberatus Kazungu, alisema halmashauri hiyo imepata hati safi kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, huku hoja zikiwa ni 22, hoja 17 zikiwa ni za mwaka 2022/23 na hoja 12 ndio zilizobaki na 11 zimetekelezwa na moja ipo katika hatua ya utekelezaji.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Dadi Kolimba, alitaka usimamizi mzuri wa kazi na kufuata hoja zilizopo awali, ikiwamo hoja za magari kutengenezwa na mifumo ya afya kufanya kazi na ushauri wa Mkaguzi wa ndani wa hesabu uzingatiwe.

"Lazima kuhakikisha mnaimarisha kitengo maalumu cha ukaguzi ili kupunguza hoja na maoni ya mkaguzi wa ndani," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live