Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanayotokana na sekta ya madini yanatokana na zao la dhahabu huku madini ya viwandani na ujenzi yakichangia kwa kiasi kidogo.
Amesema ufinyu wa mapato yatokanayo na madini ya viwandani ni kutokana na usimamizi mbovu.
Ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mchango wa madini ya viwandani umeongezeka hadi shilingi Trilioni 1.19 kufikia mwezi Februari mwaka huu kutoka shilingi Milioni 451.6 na bado kuna uwezekano wa madini hayo kuchangia zaidi pato la Taifa.
Waziri Biteko alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Wachimbaji Wadogo wa Madini na Wadau wa Madini ya Viwandani unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.