Masoko ya kununua madini ya vito na dhahabu ya Songea na Tunduru mkoani Ruvuma, yamenunua madini yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5.5/- tangu yalipofunguliwa Mei 2019 hadi Mei 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme alisema jana kuwa katika muda huo, masoko hayo ya Tunduru na Songea yamenunua madini yenye uzito wa gramu 390,936.27.
“Mrabaha uliopatikana katika mauzo hayo ni shilingi 332,093,674.35/- , ada ya ukaguzi iliyopatikana ni shilingi 55,348,945.72/- na kodi ya huduma iliyopatikana katika kipindi hicho ni shilingi 16,604,683.72/-’’ alisema Mndeme.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imeendelea kutekeleza shughuli za kukuza sekta ya madini katika mkoa wa Ruvuma.
Alisema kuwa sekta hiyo katika mkoa huo, imekua kwa kasi katika maeneo ya uwekezaji kwenye leseni za uchimbaji, uzalishaji madini, ajira na makusanyo ya maduhuli ya serikali.
Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Nkana alitaja faida za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini kuwa ni wachimbaji kupata bei nzuri ya madini kutokana na uwazi sokoni.
Alitaja faida nyingine kuwa ni wachimbaji kuepuka hatari na matatizo waliyopata ikiwemo hasara, kwa kupokonywa na serikali au vifungo kwa sababu ya kutorosha madini kwa kuwa sasa hakuna haja ya kuyatorosha.
Nkana alitaja faida nyingine kwa ni serikali kupata takwimu sahihi za mauzo ya mazini na urahisi wa kukusanya mapato yaliyokuwa yakipotea. Alisema kuwa ili kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini mkoani Ruvuma, Serikali inajenga kituo cha umahiri kwa ajili yao.
Mndeme alitaja faida za kituo hicho kuwa ni uwepo wa takwimu za wachimbaji wadogo katika mkoa huo, upatikanaji wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo na utoaji wa mafunzo na maarifa kwa wachimbaji hao kupitia wadau.
Alitaja faida nyingine kuwa ni kuwepo mfumo wa kutathmini mashapo ya madini ili kuwa na uchimbaji wenye tija, mikopo na mitaji kwa wachimbaji wadogo, uongezaji thamani madini, masoko na utatuzi wa migogoro katika uchimbaji.