Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madini ya Tanzanite kukatwa na kusanifiwa Arusha

23634 Tanzanit+pic TanzaniaWeb

Wed, 24 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Kiwanda kidogo cha kukata na kusanifu madini ya Tanzanite kimeanzishwa jijini Arusha ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhakikisha madini yote ya vito yanayouzwa nje ya nchi yanasafishwa nchini ili yaongezwe thamani.

Kiwanda hicho kimeanzishwa na kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary na tayari kimeanza kazi ya kukata madini yote ya vito, na kwa wastani kina uwezo wa kukata na kusanifu karate 3,000 kwa mwezi.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Faizal Jumaa Shabhai akizungumza na MCL Digital, leo Jumanne Oktoba 23, 2018 amesema ameamua kukianzisha ili kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuhakikisha hakuna madini ghafi yanayouzwa nje ya nchi.

"Kuuzwa madini yaliyosanifiwa kutasaidia sana Serikali kukusanya kodi, lakini pia Taifa kunufaika zaidi na madini ya Tanzanite na mengine ya vito," amesema.

Shabhai amesema sheria ya madini ya vito pia imepiga marufuku kuuzwa madini ghafi nje ya nchi.

Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Virginia Kolumbas amesema kuanzishwa kiwanda hicho ni faraja kwao kwa kuwa hadi sasa wasichana 20 wamepata ajira.

Amesema wasichana waliopata ajira wamemaliza mafunzo ya ukataji na usanifu wa madini kutoka chuo cha ukataji madini kinachomilikiwa na Wizara ya Madini mkoani Arusha.

Mwalimu wa ukataji madini katika kiwanda hicho, Bakari Mbaga amesema wanao uwezo wa kukata na kusanifu zaidi ya kareti 3,000 kwa mwezi kama wakipata madini.

Mbaga amesema katika kiwanda hicho wanaweza kusanifu aina mbalimbali ya madini kutokana na mahitaji wa wateja.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz