Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madini, gesi vyachangia trillion 8.3/- TRA

1db42324f38b68a3aea736f2080ccfb4 Madini, gesi vyachangia trillion 8.3/- TRA

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko amesema hadi sasa mchango wa sekta ya mafuta, madini na gesi asilia umefikia takribani Sh tilioni 8.03 sawa na asilimia 33.76 ya mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Kati ya hizo, asilimia 16.7 inatokana na mafuta na gesi asilia huku asilimia 17.06 kati ya hizo, ikiwa imetokana na madini.

Waziri Biteko alisema hayo wakati akifungua warsha ya siku moja kwa madiwani wa Halmashauri ya Geita Vijijini iliyoandaliwa na Tasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi asilia (TEITI).

Alisema mafanikio hayo yanatokana na mabadiliko ya sheria ya madini, uanzishwaji wa masoko ya madini nchini sambamba na kutilia mkazo fedha za uwajibikaji wa kampuni katika jamii (CSR), ushuru wa huduma na malipo ya tozo kwa TRA.

Aliwataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na madiwani ili kumaliza migogoro ya wachimbaji wadogo katika maeneo tofauti nchini huku wakizingatia kutenda haki wakiwa watatuzi wa kwanza wa migogoro katika maeneo ya wachimbaji.

Mwenyekiti wa TEITI, Ludovick Ottu, alisema sheria ya TEITI ya Mwaka 2015 imesaidia makusanyo yanayotokana na fedha za kampuni ndani ya kipindi cha miaka 10 kuongezeka maradufu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjira, alisema warsha zinazofanyika chini ya TEITI ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Wizara ya Madini kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya Sh tilioni 1.7 kulenga kupanua uelewa wa sheria za madini katika jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, alisema mabadiliko ya sheria ya madini yameufanya Mkoa wa Geita kuwa kinara wa mapato ya madini.

Gabriel alisema hali hiyo imesaidia mkoa kuingiza takribani Sh bilioni nne kuanzia Agosti hadi Desemba mwaka jana na hivyo, kupandisha mapato ya serikali mkoani hapa hadi kufikia Sh bilioni 63.8 kwa mwaka 2020.

Chanzo: habarileo.co.tz