Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madalali wa nyumba, viwanja kulipa kodi

33f64edf49647fccafebb1afbbb70585.jpeg Madalali wa nyumba, viwanja kulipa kodi

Thu, 27 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imebaini uwepo wa madalali na kampuni zisizo rasmi zinazodaiwa kuchochea migogoro na upandishaji holela wa bei ya ardhi.

Hivyo kuanzia mwaka ujao wa fedha watatambuliwa rasmi ili pamoja na mambo mengine, walipe kodi ya serikali.

Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi aliyasema hayo jana bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.

Lukuvi alisema watu na kampuni hizo wanafanya shughuli zinazohusiana na sekta ya ardhi ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuratibu mauziano ya viwanja, mashamba na nyumba.

“Wizara imebaini uwepo wa madalali wasio rasmi zikiwemo pia kampuni zinazofanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi kama vile kusimamia na kuratibu mauziano ya viwanja, mashamba na nyumba.

“Hali hii isiyoratibiwa imekuwa ikisababisha migogoro ya ardhi, upandishaji holela wa bei, kutolipa kodi za serikali na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na miamala inayofanyika baina ya wadau,” alisema Lukuvi.

Aliongeza, “hivyo imefika wakati sasa wa kuwatambua madalali wanaofanya shughuli hizo ili kuwawekea utaratibu maalum/mahsusi. Wizara imeandaa rejista pamoja na vigezo vitakavyozingatiwa katika kuwatambua madalali wote wanaojihusisha na shughuli za sekta ya ardhi.

Lukuvi alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, wizara itaandaa mwongozo/kanuni utakaoweka utaratibu wa kuratibu kazi za madalali hao ili wasiendelee kuwaumiza wananchi, kukwepa kodi na wafanye kazi kwa mujibu wa sheria.

Katika kuimarisha ukusanyaji, uchakataji na utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, alisema wizara itasimika kwa awamu mfumo unganishi wa taarifa za ardhi (ILMIS) katika ofisi za ardhi za mikoa na kuendelea kuimarisha mfumo huo katika ofisi za ardhi za halmashauri.

Alisema wizara itaongeza juhudi katika kuhuisha mifumo ya ukusanyaji maduhuli, uhakiki wa nyaraka za umiliki ardhi ili zilingane na taarifa za NIDA, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na kuimarisha miundombinu.

“Ardhi ni rasilimali kuu kwa jamii na matumizi yake ni mtambuka hivyo maendeleo katika sekta mbalimbali nchini yanategemea ardhi. Wizara itaendelea kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi hatua ambayo ni suluhisho la kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi.

“Serikali itaendelea kutambua na kuhakiki uwekezaji katika ardhi ili kutambua mchango wake katika uchumi wa nchi,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa katika muda

wa kati wa miaka mitano, wizara inalenga kupima takribani asilimia 37 ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji, makazi, biashara na matumizi mengine ya ardhi.

Aidha, alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, wizara imepanga kujenga mfumo utakaorahisisha utekelezaji wa kazi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.

“Mfumo huo pamoja na mambo mengine, utawezesha utunzaji wa kumbukumbu za mashauri yanayohusu ardhi, ufunguaji wa mashauri mapya, ufuatiliaji wa mashauri na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa njia ya mtandao,” alieleza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz