Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machungu ya kufungwa Kiwanda cha Chai Mponde kwa miaka 5

34746 Pic+kiwanda Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bumbuli. Kwa upande wa Juliana Katua (30), hakuna maneno yanayotosha kuelezea machungu na kukata tamaa kulikosababishwa na kufungwa kwa Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichopokatika Tarafa ya Bumbuli, Lushoto, Tanga kwa miaka mitano mfululizo.

Mama huyo wa watoto watatu, anawakilisha sauti ya wanawake zaidi ya 100 waliotelekezwa na waume zao kutokana na ugumu wa maisha uliosababishwa na kufungwa kwa kiwanda hicho kilichokuwa chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa familia zaidi ya 3,000 katika Halmashauri ya Bumbuli.

Kufungwa kwa kiwanda hicho Mei 26, 2013 baada ya kuibuka mgogoro mkubwa kati ya wakulima na mwekezaji aliyekuwa anakiendesha, kulisababisha pia watoto kuacha kuendelea na masomo baada ya kipato cha wazazi wao kuyumba.

“Mume wangu amenikimbia na sijui yuko wapi mpaka sasa. Sipati simu wala salamu kutoka kwake, watoto wetu wanasoma na sina wa kunisaidia,” anasema Katua.

Kusimama kwa Kiwanda cha Mponde kumesababisha wakulima katika kata 14 kati ya 18 zilizopo katika Wilaya ya Lushoto kuishi kwenye lindi la umaskini baada ya kukosa soko la kuuza majani mabichi ya chai.

“Watoto wameshindwa kuendelea na masomo na wengine wanasoma kwa shida sana. Wanaume wametukimbia. Kufungwa kwa kiwanda hiki ni maumivu sana kwa jamii nzima ya wana Bumbuli,” anasema mkulima mwingine wa chai katika Kijiji cha Mponde, Joyce Mahunda.

Hivi sasa baadhi ya wanawake waliotelekezwa na waume wameamua kujiingiza katika kazi ya kugonga mawe kama chanzo mbadala cha mapato.

Kiwanda cha Chai Mponde kilifungwa Mei 26, 2013 baada ya kuibuka mgongano mkubwa wa kimasilahi kati ya wakulima wadogo wa chai na mwekezaji aliyekuwa anamiliki asilimia 50 ya kiwanda hicho, Yusufu Mulla.

Habari njema kuhusu kiwanda hicho ni ile ya Novemba Mosi mwaka jana wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotangaza kumalizika kwa mgogoro huo akisema Serikali imekichukua na kuamuru kianze uzalishaji.

Hata hivyo, uamuzi huo umekuja wakati madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na hata kisaikolojia yamekwishatokea na kuacha makovu ambayo yatachua muda mrefu kufutika.

Hadi kilipokuwa kinafungwa, kiwanda hicho kilikuwa na uwezo wa kusindika kilo 25,000 za majani mabichi ya chai kwa siku wakati uwezo wake halisi ulikuwa kusindika kilo 70, 000 za majani mabichi kwa siku hivyo kushuka kwa asilimia 35 ya uwezo wake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Balangai, Omary Achi anasema amekuwa akipokea kesi nyingi zilisababishwa na kuporomoka kwa kipato na hali duni za maisha kutokana na kufungwa kwa kiwanda.

Thereza Mpemba aliyekuwa akisoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Msongolo alijikuta akikatisha ndoto yake ya kuendelea na masomo mwaka 2015 na kuolewa baada ya baba yake aliyekuwa mwajiriwa wa kiwanda hicho kulazimika kukaa bila kazi baada ya kiwanda kufungwa.

“Ilinibidi niache shule niende kuolewa kwa sababu ya kukosa ada ya shule maana baba yangu tangu kipindi hicho kipato chake kimeporomoka na uchumi wa famlia kuyumba,’’ anasema Theresia, ambaye kwa sasa ana watoto wawili.

Anasema ana hofu kuwa hali hiyo itawapata wadogo zake huku akiomba Serikali iharakishe kuanza kwa uzalishaji katika kiwanda hicho ili kupoza machungu ya wengi.

Diwani wa Mponde, Edwin Mahunda anasema miaka mitano ya kufungwa kwa kiwanda hicho imekuwa ya mateso makubwa kwa wananchi wengi wa kata hiyo, huku akieleza kuwa uamuzi wa Serikali kwa kukirudisha mikononi mwake umeleta tumaini jipya kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Wakulima wa Chai Korogwe na Lushoto, Almasi Shamshami anasema wakulima wamepata hasara kubwa kiuchumi kwa kukosa soko la kuuzia majani mabichi ya chai kwa miaka mitano.

Anasema, hadi sasa idadi ya wakulima wa chai waliothirika moja kwa moja na mgogoro huo ni 3,908.

“Pato la kila mkulima mwenye eneo la nusu hekta kwa mwezi wakati kiwanda kilikuwa kinafanya kazi lilikuwa Sh180,000,” anasema.

Kabla ya mgogoro huo, jumla ya hekta 1,951 zilikuwa zikitumika kuzalisha chai na hasara halisi kwa wakulima inakadiriwa kufikia Sh 702.3 milioni kila mwezi wa uchumaji majani.

Takwimu zinaonyesha kuwa Halmashauri ya Bumbuli imekuwa ikipoteza ushuru wa Sh36 milioni kila mwaka utokanao na usindikaji wa majani ya chai.

Hii ina maana kuwa halmashauri hiyo imepoteza zaidi ya Sh180 milioni za ushuru wa chai katika kipindi ambacho kiwanda kimefungwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, George Haule anasema kufungwa kwa kiwanda hicho kumesababisha uzalishaji wa chai kushuka baada ya wakulima kukata tamaa.

Anasema hali hiyo imesababisha pia takribani hekta 1,951 zinazotumiwa na wakulima wadogo kuzalisha chai kutotumiwa ipasavyo.

“Hii imeleta tishio la kufa kwa kilimo cha chai katika halmashauri na wilaya kwa ujumla. Njia pekee ya kunusuru kilimo cha chai ni kwa kiwanda hicho kuanza uzalishaji mara moja,” anasema Haule.

Ukiacha Mponde, viwanda vingine vilivyopo sasa havina uwezo mkubwa wa kusindika majani mabichi ya chai. Haule anasema kati ya kilo 400 na 600 za majani mabichi chai zinaharibika kila siku kwa kushindwa kufikiwa na magari ya viwanda hivyo.

Msimamizi wa chai kwenye vituo vya kukusanyia, Omari Bakari anasema chai nyingi huharibikia shambani kwa sababu magari hutokea mara mbili kwa wiki badala ya siku tano za wiki kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa Kiwanda cha Mponde.



Chanzo: mwananchi.co.tz