Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machinjio Vingunguti kuingiza bilioni 4/-, kutoa ajira 3,000

Fee3b0eee28ca0c30af93032b1052c13 Machinjio Vingunguti kuingiza bilioni 4/-, kutoa ajira 3,000

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JIJI la Dar es Salaam linatarajiwa kuingiza zaidi ya Sh bilioni 4 kwa mwaka kutoka kwenye Machinjio ya kisasa ya Vingunguti, yanayotarajia kuanza kazi Machi mwaka huu.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri amesema kuwa uongozi wa jiji hilo, umefanya mchakato wa kuagiza magari maalumu ya kubebea nyama kwa ajili ya kuzisambaza kwa walaji.

Shauri alilieleza HabariLEO jana kuwa machinjio hiyo itakapoanza kazi, itatoa ajira 3,000 za moja kwa moja na tayari mafunzo kwa baadhi ya wahudumu 150 wa mahali hapo yameanza.

"Matarajio wakati wowote ndani ya mwezi huu kazi rasmi za uchinjaji wa ng’ombe ndani ya machinjio hii inaweza kuanza, kinachosubiriwa kwa sasa ni kumalizika kwa mafunzo ya wafanyakazi wa machinjio yanayoendea kutolewa, ila kuhusu ujenzi huo kwa asilimia kubwa kila kitu kimeshakamilika" alisema.

Shauri alisema kwa kuzingatia matakwa ya walaji wa nyama, ng'ombe watachinjwa asubuhi hadi jioni ili kuondoa msongamano unaosababishwa na utamaduni wa kuchinja ngombe usiku pekee.

Alisema wanatarajia kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama katika eneo hilo, kitakachokuwa chini ya kikundi cha akina mama.

Shauri alisema kiwanda hicho kitazalisha nyama za aina mbalimbali zikiwemo za kusaga na zingine kulingana na matakwa ya mlaji kisha kuziingiza sokoni.

"Kiwanda hiki kitakachokuwa kikisimamiwa kwa karibu na uongozi wa Jiji, malengo yake ni kuhakikisha kinazalisha nyama aina tofauti tofauti yakiwemo maini, nyama ya nundu na zinginezo kisha kuziweka katika vifungashio maalumu na kumfikia mteja mahali alipo, lakini pia kuzipeleka katika 'Supermarket' kwa ajili ya kuuzwa, huu ni uwekezaji ambao utaongeza ufanisi wa machinjio yetu" alisema.

Shauri alisema pia kutokana na uchunaji wa kisasa jiji hilo na wachinjaji, wanatarajia kuvuna ngozi bora ya ng'ombe, mbuzi , na kondoo hivyo watapata soko zuri tofauti na ilivyokuwa awali.

Aliwataka wafanyabiashara wa nyama wa mkoa wa Dar es Salaam, wajiandae kutumia fursa za machinjio hiyo ya kisasa kwa kuweka mazingira mazuri yatakayowawezesha wananchi kupata nyama kwa ubora uleule unaozalishwa kutoka machinjioni hapo.

Shauri pia aliwataka wauzaji na wasafirishaji wa ng'ombe, mbuzi, na kondoo kutoka mikoani, wajiandae kuongeza idadi ya mifugo inayoletwa Dar es Salaam, kwa kuwa mazingira ya machinjio hiyo kwa sasa yamekuwa bora kuwezesha zaidi ya mifugo 5,000 kuchinjwa kwa siku.

Chanzo: habarileo.co.tz