Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machinga walalamika vitambulisho kielektroniki

C39b2c61ce1b805a7d64a6bbfec4d26f Machinga walalamika vitambulisho kielektroniki

Mon, 24 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAFANYABIASHARA wadogo maarufu kwa jina la Machinga wamedai kuwa utaratibu wa sasa kupata vitambulisho vya wajasiriamali kielektroniki ni mgumu kwao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wadogo Mkoa wa Morogoro (SHIUMA) , Fustine Francis alisema mfumo wa uombaji wa njia ya kieletroniki umekuwa kikwazo wa wafanyabiashara wadogo.

Francis alisema wafanyabiashara wadogo wengi hawana simu janja na pia hawana uwezo wa kuweka vifurushi vitakavyowawezesha kujisajili kielektroniki.

"Nikiwa Mwenyekiti wao Mkoa wa Morogoro nimekuwa nikipokea simu za kuulizia vitambulisho hivi kama serikali imevileta , lakini vimeletwa kwa mfumo tofauti na mwaka jana ( 2020) na kumtaka mfanyabiashara ajisajili yenye mwenyewe na hilo ndilo tatizo la kusuasua kuchukuliwa kwa vitambulisho " alisema Francis .

Aliiomba serikali iangalie upya namna ya kuwezesha wafanyabishara wadogo ikiwa ni pamoja na kusajili maombi kama ilivyokuwa katika uandikishaji kitambulisho cha taifa ama cha mpiga kura.

Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro sehemu ya uchumi na uzalishaji, Dk Rozalia Rwegasira alisema Machi mwaka huu mkoa huo ulipokea vitambulisho vya kieletroniki 58,000 kutoka serikali kuu na vikapelekwa kwenye halmashauri tisa za mkoa huo.

Rwegasira alisema hadi Aprili 20 mwaka huu ni vitambulisho 273 ndivyo vilivyokuwa vimelipiwa na kati ya hivyo vilivyokuwa vimechapishwa ni sita tu. Machinga wanapata vitambulisho hivyo kwa kulipa sh 20,000.

Alisema utaratibu wa uombaji wa vitambulisho ni tofauti na mwaka jana na kwamba mwaka huu ni kwa njia ya mfumo wa kieletroniki hivyo mfanyabiashara mdogo anapaswa kutumia simu ya mkononi kutuma maombi.

Rwegasira alisema maombi hayo ni kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na programu tumizi ya mfumo wa machinga, na mfumo huo utakuwa na uwezo wa kutoa namba ya kumbukumbu ya maombi na namba ya malipo baada ya taarifa za muombaji kukamilika .

Alisema maombi ya kitambulisho yanaweza kufanyika kwa njia ya mwombaji ambaye ana kitambulisho cha taifa au leseni ya udereva, ataweza kujisajili mwenyewe kupitia mtandao wa www.tamisemi.go.tz au simu janja ya mkononi kwa kupakua Machinga App na kujisajili mwenyewe.

"Kwa wale ambao watashindwa kutumia njia hizo, wanatakiwa kwenda katika ofisi za Halmashauri zilizo jirani yao ili waweze kupata msaada wa kujisajili" alisema Rwegasira.

Katibu Mkuu Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Riziki Shemdoe alilieleza HabariLEO kuwa ofisi yake inaandaa taarifa kuhusu suala hilo.

“Tunawaandalia taarifa nzuri ili ikienda kwa jamii isiwe na mkanganyiko. Vuteni subira,” alisema Shemdoe.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa MlipaKodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema mfumo huo umeongeza wigo kwa wafanyabiashara kupata vitambulisho.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania, Ernest Masanja alisema wafanyabiashara wadogo wanatumia kwa kiasi kidogo simu janja zinazoweza kutumika kujisajili kupata vitambulisho hivyo.

“Tunaishauri serikali kwanza kuwashirikisha viongozi wote wa wamachinga nchi nzima katika ngazi ya mkoa, wilaya na katika ngazi ya masoko ili iwe rahisi kufundishana popote walipo. Hii itasaidia kueneza elimu hiyo kwa haraka na kuwawezesha kupata vitambulisho hivyo haraka,”alisema Masanja.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Mkoa wa Arusha, Amina Njoka alisema mabadiliko yaliyofanywa katika upatikanaji wa vitambulisho yana nia nzuri lakini mfumo unaotumika ni mgeni kwa wajasiriamali.

“Wamachinga hawakuzoea mfumo huo kwa sababu mwanzo haukuwa hivyo, wengine hawana simu janja na hata walizo nazo hawajui namna ya kujisajili hivyo itachelewesha mchakato, hivyo ingekuwa vizuri kuwashirikisha wamachinga katika utoaji wa elimu ili kurahisisha kazi,” alisema Njoka.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira akizungumza kabla ya kustaafu alisema ofisi yake inatambua changamoto za mfumo mpya wa upatikanaji wa vitambulisho vya Machinga ikiwa ni pamoja na baadhi yao kutokuwa na simu janja na wengine kutokuwa na uwezo wa kupata intaneti.

Alisema ofisi yake ilimuagiza mtumishi wa TRA anayehusika na elimu kwa umma atoe mafunzo kwa viongozi wa Machinga ili kuondoa malalamiko kuhusu utaratibu wa kutumia simu kujisajili.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wafanyabiashara Wadogo Tanzania (VIBINDO), Gastoni Kikuwi amesema utaratibu wa kuwataka wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) kuomba vitambulisho vya biashara kupitia usajili wa mtandaoni ni ‘mzigo’ kwa wafanyabiashara.

Kikuwi alisema utaratibu huo unawapa shida kwa kuwa si wafanyabiashara wote wana uzoefu wa kutumia mitandao hiyo hivyo alishauri utumike utaratibu wa awali kugawa vitambulisho hivyo.

“Binafsi nimejaribu kujisajili kupitia mfumo huo nikashindwa kutokana na usajili huo kuwa na mlolongo mrefu, kimsingi hii ni changamoto kubwa inayokwenda kuwafanya wafanyabiashara wakashindwa kupata vitambulisho hivyo, tunaomba mamlaka inayohusika iliangalie suala hili kwa kina kuondoa usumbufu,” alisema Kikuwi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Donald Nsoko alisema mfumo mpya wa usajili wa vitambulisho vya mjasiriamali umeonekana kuwa kikwazo katika kufanikisha jambo hilo.

Nsoko alisema ili kuikabili changamoto hiyo tayari watendaji wamepewa maelekezo na mafunzo ya namna ya kutumia mfumo, kwa kuwa haujawa rafiki kwa walengwa.

"Bado huu mfumo ni mpya tofauti na ule wa zamani ambao ni wa njia ya makaratasi ulikuwa rahisi na uliwahamasisha wengi kujiunga kwani kipindi kile tulikuwa tunawafuata wafanyabiashara sehemu zote tunawasajili lakini kwa sasa mtu mwenyewe anatakiwa aingie mtandaoni afanye usajili”alisema na kuongeza;

"Kwa kweli imekuwa ngumu sana kwa wafanyabishara wengi kwa maana ukute mfumo wenyewe ni mgeni kwake ama haujui kwa hiyo ni changamoto na kasi ya uandikishaji haijawa nzuri nadhani siyo kwa halmashauri yetu tu ni kwa maeneo yote ila kuanzia jumatatu timu iliyoundwa itaanza rasmi kufuatulia.

Imeandikwa na John Nditi (Morogoro), Yohana Shida (Geita), Evance Ng’ingo, Selemani Nzaro, Oscar Job na Halima Mlacha (Dar es Salaam).

Chanzo: www.habarileo.co.tz