Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machinga kufunga shughuli kuomboleza

8f5a10324539f31bc7ba3d0f86b794ee Machinga kufunga shughuli kuomboleza

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Umoja wa Machinga Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi amesema leo hawatafanya biashara zao kwa ajili ya kushiriki kuuaga mwili wa Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam.

Alisema Rais Magufuli amewafanyia mema mengi kama wananchi wanyonge, hivyo watafanya hivyo kwa heshima yake kwani alikuwa mtetezi wao katika kipindi chote cha uhai wake.

Mponzi aliwataka machinga wanaofanya biashara zao katika masoko yote ya mkoa huo kushiriki kikamilifu kuuaga mwili wa kiongozi huyo.

Akizungumza na wafanyabishara ndogo ndogo, alisema kuwa kwa upande wao wataendelea kumuenzi Rais Magufuli kutokana na mchango mkubwa aliouonesha kwa machinga wote nchini.

"Kwa siku hiyo ya Jumatatu (leo) kama serikali ilivyotangaza kuwa ya mapumziko na sisi hatutafanya shughuli yoyote ya kimachinga, bali tutahakikisha kila mmoja wetu anashiriki kumuaga mpendwa wetu Rais Magufuli,"alisema.

Naye Baraka Mrisho ambaye ni Mwenyekiti wa wamachinga Dodoma mjini amewataka machinga kutoa ushirikiano kwa serikali katika kipindi hiki ambacho wapo kwenye majonzi makubwa ya kuondokewa na Rais Magufuli na kusema wanatakiwa kumuenzi kwa vitendo.

Awali akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna amewataka machinga hao kuwa na imani kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika utendaji wake kwa kuwa atawaboreshea mazingira yao na kuweza kutoka kwenye maisha ya umasikini na kuongeza mitaji.

Alisema kuwa imani hiyo inatokana na utendaji mkubwa alionao wa Rais Samia ambaye pia amekuwa akitoa mchango mkubwa kuhakikisha wafanyabiashara hawabughudhiwi bali wanafanya kazi zao kwa uhuru.

Chanzo: www.habarileo.co.tz