Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabosi 40 wa kampuni, mashirika wawekwa kikaangoni

85663 Pic+hazina Mabosi 40 wa kampuni, mashirika wawekwa kikaangoni

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mashirika ya umma 40 nchini Tanzania yanayojiendesha kibiashara yakishindwa kutoa gawio kwa Serikali, Msajili wa Hazina nchini humo, Athuman Mbutuka amewataka wenyeviti na watendaji wakuu wa mashirika hayo kujitathimini kama wanafaa kuendelea kuongoza mashirika hayo.

Mbutuka ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 24,2019 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika taasisi, mashirika na kampuni ambazo Serikali ya Tanzania ina hisa.

Amesema kati ya mashirika 81 yanayojiendesha kibiashara, mashirika 40 yameshindwa kutoa gawio kwa sababu yanajiendesha kwa hasara.

“Natoa rai kwa wenyeviti na watendaji wa mashirika hayo wajitathmini kama wanatosha kuongoza mashirika hayo,” amesema Mbutuka huku akiyataka mashirika ya huduma nayo kupunguza utegemezi kwa Serikali.

Msajili huyo amesema kiwango cha makusanyo ya gawio kwa serikali kimeongezeka kutoka Sh161.04 bilioni mwaka wa fedha wa 2014/15 mpaka kufikia Sh1.05 trilioni mwaka 2018/19 ikiwa ni ongezeko la asilimia 552.

Mbutuka amesema ofisi yake ilifanya uhakiki wa mali zinazomilikiwa na Serikali na kubaini kuna nyumba 337, viwanja 140, mashamba makubwa 10 na kampuni mbili. Amesema mali hizo zote zimerudishwa serikalini.

“Tulibaini kuna kampuni mbili ambazo hazipo kwenye orodha yetu, kuna kampuni ya Songwe Water Company ambayo Serikali inamiliki kwa asilimia 100 na kampuni ya Liquid Storage ambayo Serikali ina hisa ailimia 40,” amesema.

Amebainisha katika kuboresha utendaji wa mashirika ya umma, mashirika 15 yaliunganishwa na kubaki mashirika manane pekee. Amesema hiyo imepunguza gharama za uendeshaji kwa sababu kila shirika lilikuwa na mtendaji mkuu wake.

Chanzo: mwananchi.co.tz