Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam yafungua fursa lukuki

5b009bb517e3c53822fd939974b57488 Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam yafungua fursa lukuki

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MRADI wa Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) unaohusisha ujenzi wa gati namba moja hadi nane umefikia asilimia 95 ya ujenzi wake huku uzinduzi rasmi wa mradi huo ukitegemewa kufanywa mapema Juni, mwaka huu (2021).

Hatua hiyo imekuja baada ya mradi huo mkubwa wa thamani ya Sh bilioni 337 kuanza kazi mwishoni mwa 2017 baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kusaini mkataba na Kampuni ya M/s China Habour Engineering Company Limited inayotekeleza kazi hiyo.

Katika utekelezaji wake, gati namba moja hadi tano ujenzi wake umekamilika ikiwa ni pamoja ujenzi wa gati mpya maalumu kwa ajili ya kuhudumia meli za magari (RoRo Berth) kwenye bandari hiyo, iliyopewa jina la gati namba nane, ambayo imeshaanza kufanya kazi na kwa tayari meli kadhaa kutoka nje zimeshatia nanga na kushusha magari.

Baadhi ya meli hizo ni pamoja na meli ya Lavender Ace iliyotia nanga Januari 19,2021 bandarini hapo ikiwa na magari kadhaa kutoka nchi za Asia na kwingineko ambapo pia kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema, hivi sasa fursa zimeongezeka katika bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kutumika kama kiungo cha kupitishia bidhaa na shehena za nchi nyingine.

Lema akizungumzia ufanisi katika bandari hiyo baada ya kuanza mradi huo wa DMGP, utekelezaji wake umefikia asilimia 90 na kwamba gati namba moja hadi nne zimeshakamilika na zinatumika hivi sasa na meli za ukubwa wa aina yotote kutoka nje zina uwezo wa kuingia bandarini hapo kushusha na kupakia mizigo, bila kufaulisha kwenye meli ndogo.

Alisema hivi sasa hakuna meli inayokaa foleni baharini kusubiri meli nyingine ziondoke bandarini ili nazo zipate nafasi ya kushusha mizigo na kuwa meli zote kwa sasa zinapoingia nchini huenda bandarini hapo moja kwa moja na kushusa shehena iliyobeba bila vikwazo na kwa muda mfupi kisha huondoka.

“Hakuna tena foleni hapa bandarini, meli ikiingia inakuja moja kwa moja, ukikuta meli imetia nanga baharini kule maeneo ya Coco beach, ama ina mambo mawili, moja labda haijamaliza kulipa tozo na ada mbalimbali za kutumia bandari hii na jingine unakuta meli hiyo ina mizigo ya watu au waagizaji tofauti ambapo baadhi yao wameshalipia tozo zao na wengine bado hivyo inabidi hadi wote wamalize ndio waingie, lakini ile foleni ya zamani kusubiri nafasi haipo’’, anasema Lema.

Akitoa mfano anasema, katika gati jipya la magari (RoRo Berth), ufanisi umeongezeka mara dufu na kuwa hivi sasa magari hutolewa kwa wingi kwa wakati mmoja ambapo kwa saa moja zaidi ya magari 72 hushushwa melini, wakati awali ilikuchuka muda mrefu zaidi ya huo.

“Hii imesaidia waagizaji wengine hutuoa magari yao muda mfupi tu baada ya meli kushusha, ufanisi umeongezeka, wizi wa vitu vya magari umeondoka pia hakuna ajali tena za bandarini na bado tunapata mizigo ya kwenda nchi nyingine kama Afrika Kusini”, anasema Lema.

Anabainisha kuwa kwa sasa meli ya magari hutumia siku moja hadi mbili tu kushusha magari kisha huondoka wakati awali ilitumia zaidi ya siku tano na wakati mwingine magari ilibidi meli ianze kushusha baadhi katika bandari ya Mombasa, Kenya kisha ndio ije Dar es Salaam kwa sababu ya foleni na kushindwa kuingia bandarini kwa kuwa gati na kina cha maji kilikuwa kidogo kuruhusu meli kubwa kutia nanga.

Akizungumzia gati namba moja hadi tano, Lema alibainisha ulihusisha kuongeza eneo la kupakia na kupakua mizigo na kuongeza kina cha maji mpaka kufikia mita 14.5 kutoka mita 11 za mwanzo, ambako sasa meli kubwa hadi zenye urefu hadi wa mita 300 zitakuwa na uwezo wa kuingia bandarini hapo.

Hivi sasa meli hizo zimeanza kuingia na gati hizo zinatumiwa na meli zenye mizigo tofauti kushusha mizigo mchanganyiko ikiwemo shehena za mbolea, klinka, ngano na mizigo mingine.

Mwishoni mwa mwaka jana, gati hizo zilianza kutumika ambapo meli kadhaa zilitia nanga ikiwemo meli ya Ever Alliance iliyotoka Oman, ikiwa na malighafi ya klinka inayotumika kutengeneza saruji, ilikuwa imebeba tani zaidi ya 45,000 na shehena hiyo ilipakuliwa ndani ya siku tano tu wakati awali ingepakuliwa hadi siku 15.

Kuhusu ujenzi wa gati namba tano hadi saba, ujenzi wake unaendelea na kwamba utakamilika mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, ili uzinduzi ramsi wa serikali wa mradi huo ufanywe Juni, 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko anabainisha kuwa maboresho hayo kwa ujumla yametokana na mpango wa muda mrefu wa miaka 20, ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2009 unaopanga bajeti zao za miaka mitano mitano ndani ya mpango mkuu.

Katika uboreshaji wa bandari nchini, TPA iliweka mpango wa kuboresha bandari zake zote, ikiwemo ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na nyingine lengo likiwa ni kuongeza tija na ufanisi wa bandari lakini pia bandari hizo ni kitovu cha uchumi wa nchi hivyo ni lazima zifanyiwe mageuzi mapana kukuza uchumi.

Akizungumzia kwa ujumla ufanisi na bandari hiyo baada ya maboresho kuanza, Kakoko anasema kwenye gati ya magari hivi sasa wana uwezo wa kushusha meli yenye magari hadi 1,000 kwa wakati mmoja wakati awali ilikuwa na uwezo wa kushusha magari 500 tu.

Aidha, kwenye meli zinazobesha shehena kichele, hivi sasa bandari hiyo ina uwezo wa kupokea meli kubwa za hadi meta 300 wakati awali ilikuwa na uwezo wa kupokea meli za ukubwa hadi meta 240 na kuwa kwa upande wa makasha meli zinazobeba hadi makasha (containers) 3,000 na wakati mwingine hadi 4,500 zinaweza kupakuliwa wakati zamani ilikuwa ni makasha 400 pekee.

“Magati hayo namba moja hadi 4 kwa sasa yana uwezo wa kuruhusu meli kubwa kuingia, tumeongeza kina cha maji kutoka meta 11 hadi 14.5 na kama maji yakijaa kina huongezeka hadi kufikia meta 19 na hivyo meli zenye ukubwa wowote zinauwezo wa kutia nanga na kupakuliwa shehena iliyopo ndani ya siku chache tu’’, anaeleza Kakoko.

Wakati Kakoko akisema hayo, Ofisa Mkuu Idara ya Midaki (scanner) wa TPA, Mtani Rugina anabainisha kuwa maboresho ya bandari nchini yameleta ufanisi kwa sababu mamlaka imefunga midaki 11 ya kisasa katika bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga inayopiga picha makasha na kubainisha chochote kilichomo ndani hata kama kimefichwa kiasi gani hubainika.

“Midaki hizo ni za kisasa na zinabaini vitu vyote vilivyomo ndani ya makasha hakuna kinachopita bila kubainika, udhibiti ni wa hali ya juu na kama kuna chochote chenye kasoro hubainishwa na kama ni mionzi zaidi ya kiwango hujulikana na mamlaka husika hutaarifiwa mara moja na kuja kushughulika nao”, anasema Rugina.

Kwa upande wa uboreshaji wa gati ya kupakilia mafuta ya Kurasini (KOJ), Kaimu Meneja wa KOJ, Sixtus Kavia anasema hivi sasa flow mita za kupokelea mafuta bandarini hapo zipo 19 mpya na za kisasa zilizosaidia kuongeza ufanisi na kuongeza mapato ya bandari.

Kavia anasema, tangu kuanza kutumia kwa mabomba hayo mapya ya kupokelea mafuta bandarini, ufanisi umeongezeka na hiyo inawahakikishia tena kuongeza fursa ya kusafirisha mafuta kwa kutumia bomba la mafuta la Tazama linaloelekea nchini Zambia.

Hizo ni baadhi tu ya fursa zinazopatikana baada ya maboresho ya bandari kupitia mradi wa DMGP ambao umedhamiria kuboresha bandari zote nchini ikiwemo ya Mtwara ambayo ukarabati wake unaendelea, bandari ya Tanga na bandari nyingine nchini ili ziongeze ufanisi na kuhudumia eneo kubwa zaidi.

Chanzo: habarileo.co.tz