Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maboresho muundo wa mashirika ya umma waanza rasmi

Nehemia Mchechu Leo Maboresho muundo wa mashirika ya umma waanza rasmi

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza utekelezaji wa mageuzi kwenye muundo na utaratibu wa kusimamia mashirika na taasisi za umma, ili kuongeza tija kwenye utendaji wake.

Sehemu ya utekelezaji wa mageuzi hayo kama yalivyotangazwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu ni kuhusu kuajiri na kufukuza watendaji wakuu wa mashirika ya umma.

Agosti 20, 2023, Mchechu alizungumza mbele ya wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma jijini Arusha, alisema kufanya hivyo ni kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi hizo.

Hata hivyo, Desemba 15 mwaka jana ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, Serikali iliyaunganisha mashirika na taasisi 16, pamoja na kufuta mengine manne yaliyokuwa chini ya Msajili wa Hazina.

Tangazo la ajira lililotolewa na ofisi hiyo kwenye gazeti la Serikali la Daily News, Januari 8, 2024, Msajili wa Hazina ametangaza nafasi za wajumbe wa bodi katika mashirika ya umma waliobobea katika sekta mbalimbali ikiwemo mafuta na gesi, madini, nishati, taasisi za fedha pamoja na utalii.

Ofisi ya Msajili imetoa hakikisho kuwa itatenda haki katika kuchagua wenye sifa na waliotimiza vigezo kisheria na kwa mujibu wa taratibu zinazosimamiwa na shirika husika.

Kwa mujibu wa Mchechu, hayo yote yanatekeleza dhamira yao ikiwa ni kuhakikisha mchango endelevu wa taasisi na mashirika ya umma kwa maendeleo ya Taifa kwa kuzingatia ubora wa utendaji kazi, huduma na uwezekano wa kibiashara.

“Bodi ni chombo cha juu chenye jukumu muhimu katika kuongoza mwelekeo wa kimkakati na utawala wa taasisi hizi. Kwa hivyo, kuajiri mchanganyiko wa wajumbe wa bodi ni muhimu kwa shirika lolote lenye malengo ya kuwa na matokeo,”alinukuliwa akisema Mchechu.

Akitoa maoni hatua hiyo, Profesa Abel Kinyondo, mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema hatua hiyo ni muhimu katika kufikia malengo huku akitoa angalizo katika mchakato wa kuwaajiri wajumbe hao.

Profesa Kinyondo amesema jambo hilo linamaanisha uwazi katika mchakato wa upatikanaji wa watendaji wa uamuzi.

Kinyondo amesema utaratibu wa kuwapata watu bora kama lengo la hatua hiyo, endapo usipotumika basi itakuwa haina maana.

“Msajili ameona umuhimu wa kuweka uwazi wa kuwatafuta wajumbe lakini tukumbuke mjumbe hausiki katika shughuli za kila siku za taasisi au shirika, kwa bahati mbaya viongozi bado wanateuliwa.

“Hivyo angalizo langu tushuke hadi ngazi ya uongozi ambayo inahusika na shughuli za kila siku na wenyewe watafutwe kwa njia hiyo. Asiwepo mkuu wa taasisi ambaye anateuliwa. Akiteuliwa anakuwa hajapitia mchakato wa mashindano.

Profesa Kinyondo ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa hatua hiyo muhimu ya uwazi wa kuwapata wajumbe hao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live