Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Maboresho bandari ya Dar  yataongeza shehena maradufu’

A976e282e31f562b084434858f291afa ‘Maboresho bandari ya Dar  yataongeza shehena maradufu’

Wed, 26 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BANDARI ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kuhudumia tani za mizigo kati ya milioni 25 hadi milioni 30 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025 kutoka tani milioni 16.1 za sasa.

Uwezo huu utatokana na kukamilika kwa maboresho na upanuzi unaoendelea bandarini hapo ambao utaifanya Bandari hiyo kuendelea kuwa kiungo muhimu katika kukuza uchumi na kurahisisha shughuli za kibiashara, siyo kwa Tanzania tu bali hata katika nchi takribani nane zinazopakana na Tanzania ikiwemo Sudan Kusini.

Akizungumza na HabariLEO ofisini kwake hivi karibuni, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema, amezitaja nchi hizo kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Comoro na Sudan Kusini.

Lema anasema kiwango cha mizigo kinachohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kimeongezeka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutoka tani milioni 13.8 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani milioni 16.1 mwaka 2019/2020.

Anasema maboresho na upanuzi wa bandari hiyo yanatarajia kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo wa kuhudumia tani hizo za mizigo milioni 30 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

“Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 bandari hii ilihudumia jumla ya tani milioni 13.3 za mizigo, mwaka uliofuata, 2017/2018 ilihudumia tani milioni 14.9 na mwaka 2018/2019 tani milioni 15.7 za mizigo ya nchi hizo,” anasema Lema.

Anabainisha kuwa kuongezeka kwa kiwango cha mizigo kunachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo maboresho ya bandari kwa kuongeza kina cha gati zake kutoka mita 8.5 hadi kufikia mita 14.5.

Anasema kuongezwa kwa kina cha gati namba moja hadi gati namba saba, kumezifanya meli zenye ujazo mkubwa kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Baada ya maboresha haya ya kuongeza kina cha gati zetu hadi kufikia mita 14.5 faida ambazo tumeanza kuzipata ni pamoja na meli zenye ujazo mkubwa kuanzia tani 40,000 hadi tani 50,000 kutia nanga kwenye gati hizi ikilinganishwa na zamani ambapo zilikuwa zinakuja meli ndogo zenye ujazo wa tani 15,000 hadi tani 30,000,” anasema.

Anaongeza kwamba hata meli kubwa zenye urefu wa mita zaidi ya 200 (yaani zaidi ya viwanja viwili ya mpira) sasa zinaweza kutia nanga katika bandari hiyo.

Kukamilika na kuanza kutumika kwa gati jipya la magari na yadi ya kuhifadhia magari pia ni sababu ya kuongeza kiwango cha magari yanayoshushwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Lema anasema gati jipya linalojulikana kama gati 0 (roll in roll out) lenye urefu wa mita 320 limeongeza ufanisi katika ushushaji wa magari zaidi ya 100 kwa saa ikilinganishwa na magari 50 hadi 70 hapo awali.

“Muda unaotumika kupakua meli yenye magari na kuondoka ni siku moja na ikizidi sana ni siku moja na nusu ikilinganishwa na siku tatu zilizokuwa zikitumika hapo kabla. Kwa mfano meli yenye magari 1,100 inachukua siku moja na nusu tu kumaliza kushusha,” anasema Lema.

Akionesha takwimu namna Bandari ya Dar es Salaam inavyozihudumia nchi zisizo na bahari, Lema anasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kiwango cha mizigo ya nchi hizo inayohudumiwa na bandari hiyo kimekuwa kikiongezeka.

Anasema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 Zambia ilipitisha mzigo wa tani milioni 1.4, DRC tani milioni 1.9, Rwanda tani milioni 1.3, Burundi tani 478,000, Malawi tani 376,000, Uganda tani 140,000 na nchi zingine tani 35,000.

Mkurugenzi wa Bandari anaeleza kuwa hata mizigo ambayo zamani walikuwa hawaipati ikiwemo ya kusafirisha magari, lakini siku hizi wanaipata kupitia mizigo inayoshushwa bandarini hapo na kisha kupakiwa kwenye meli nyingine na kwenda kwenye nchi husika (Transshipment).

Aidha, Lema anasema mbali na Bandari ya Dar es Salaam, Bandari Bubu zilizoanza kurasimishwa nchini zimeiingizia Serikali mapato ya Sh bilioni 1 kwa mwaka uliopita wa 2019/2020.

Anasema bandari bubu zilizopo nchini ni nyingi na zinafikia takribani 600 pamoja na zile ambazo ziko kwenye maziwa.

Kutokana na wingi wa bandari bubu nchini, anasema Dar es Salaam wameanza kazi ya kuzirasimisha bandari hizo ikiwemo Bandari Bubu ya Mbweni.

“Kwa Dar es Salaam zipo bandari bubu nyingi lakini tumeanza kuziainisha chache kama kumi hivi, na kati ya hizi kumi tumeanza na bandari tano ikiwemo moja maarufu ambayo unaweza kuiita ‘Baba Lao’ ambayo ni Bandari ya Mbweni.

“Unapoziacha bandari bubu ziendelee kufanya kazi unahatarisha usalama kwa sababu watu wanaweza kuzitumia kupitisha magendo kuleta nchini, pia mapato ya serikali yanapotea kwa sababu wanaozitumia hawalipi kodi wala tozo zozote,” anaeleza Lema.

Anaongeza: “Bandari bubu nchini zimeingiza shilingi bilioni moja kwa mwaka uliopita. Tulikusanya kwa kutumia mashine za POS.”

Mbali na kuhatarisha usalama, Lema anasema bandari bubu pia zinaathiri uchumi wa nchi kwa sababu wanaoingiza bidhaa kupitia bandari hizi wanakwenda kushindana kibiashara na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa zao kiuhalali na kuzilipia kodi, hali inayofanya kutokuwepo kwa usawa katika soko.

Kutokana na hali hiyo, anasema Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ikaweka mkakati wa kuanza kuzisimamia bandari bubu na kukusanya mapato, hivyo wakaanza na Bandari bubu ya Mbweni, Tunguji na Kilongwe zilizopo Mafia na zinginezo.

“Hatua ya kwanza tulianza kuweka watu wetu wa kukusanya mapato, hatua ya pili tumeweka ofisi za muda na stoo kwa kutumia kontena, lakini tuna mpango wa kuendeleza miundombinu hiyo,” anasema Lema.

Mkurugenzi huyo wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio kubwa kuliko zote nchini anasema mizigo mingi inayopitishwa kwenye bandari bubu ni ya vyakula zikiwemo nazi, sukari na mazao mengine ya kilimo.

Vitu vingine vinavyosaidia kuongeza shehena ni huduma bora kwa wateja, ulinzi na usalama wa mizigo na uboreshaji wa miundombinu kutoka bandarini kwenda bara hadi nchi za jirani.

Ufanisi wa watu wanaosafirisha mizigo kwa nchi kavu, yaani wale wenye malori na umekuwa ukitoa mchango mkubwa kwa ufanisi wa bandari.

Sambamba na wenye malori, kuna mashirika ya reli kama TRL (Shirika la Reli Tanzania) na Tazara (Tanzania Zambia Railway Authority) ambao pia wamekuwa wadau muhimu kwa maendeleo ya bandari. Hali ya usafirishaji mizigo na hivyo kuvutia wengi zaidi kutumia bandari ya Dar es Salaam kunatarajia kuboreka baada ya kukamilika kwa reli ya kisasa (SGR).

Mkurugenzi mkuu wa zamani wa TPA, Deusdedit Kakoko alipata kusema: “Kimsingi, hawa wasafirishaji wa mizigo ni muhimu kuliko hata bandari yenyewe kwa sababu kama unapokea shehena halafu haitoki, huwezi kufanya biashara. Kama hawapo vilevile huwezi kupokea mzigo kwa ajili ya kutuma nje.”

Kakoko pia alikuwa anasema kwamba ufanisi wa bandari kwa maana ya kupokea mzigo kwa haraka na kuusafirisha kunapungiza gharama za bidhaa na kuboresha maisha ya wote wanaoitegemwa bandari ya Dar es Salaam

“Ukipunguza gharama, unaongeza pia uwezo wa watu kununua bidhaa,” alisema Kakoko.

Chanzo: www.habarileo.co.tz