Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maboresho PTA yatoa matokeo chanya

Bandaripic Data Maboresho PTA yatoa matokeo chanya

Fri, 21 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) yameanza kutoa matokeo chanya kwa kuongezeka kwa idadi ya meli zinazoingia nchini kwa mwezi.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamisi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kumekuwa na ongezeko la meli zaidi ya 20 kwenye wastani wa meli 50 kwa mwezi.

Akizungumza kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete, Hamissi  ameeleza kuwa kwa mwezi bandari ilikuwa ikipokea wastani wa meli 50 lakini kuanzia Novemba mwaka jana zimeanza kupanda.

Amesema Novemba ziliingia   meli 77 wakati Desemba ziliingia  meli 67 hali inayosababisha kuongezeka kwa shehena za mizigo inayoingia nchini.

Ongezeko hilo linafanya mizigo iliyoingia nchini hadi sasa kuanzia Julai 2021 kufikia tani 9.1 milioni huku lengo kufikia mwisho wa mwaka wa fedha Juni mwaka huu iwe imehudumia shehena ya mizigo tani 18 milioni.

Hamissi alieleza kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana bandari imeingiza Sh508 bilioni ambayo ni zaidi ya asilimia 50, lengo kufikia mwisho wa mwaka wa fedha ni kuingiza Sh1 trilioni.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo mafanikio hayo yametokana na uboreshwaji wa huduma ikiwamo kuhudumia kwa haraka meli zinazoingia nchini.

Kutokana na ongezeko hilo alisema kuna siku bandari inapokea hadi meli sita na jitihada zinafanyika ili zote zihudumiwe kwa haraka.

“Vifaa ambavyo tumepewa na serikali vinaendelea kusaidia kuongeza ufanisi na matokeo yake tunayaona meli zinaongezeka, mizigo mingi ya nchi jirani inapita kwenye bandari yetu.

“Hata hivyo bado haturidhishwi na idadi ya  mizigo ya nchi jirani inayopita kwetu, tunataka iongezeke zaidi kwa kuwa bandari yetu ina uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia. Tunataka mizigo zaidi ipite hapa kwetu,”

Katika kufanikisha hilo alisema bandari inaweka mikakati ya kutangaza na kuhamamisha nchi jirani kutumia bandari ya Dar es Salaam.

“Huko nyuma tulikuwa hatujatangaza sana lakini sasa tunaweka nguvu katika eneo hilo na tunavyozidi kuwahudumia vizuri wateja wetu tuna imani wanakwenda kututangaza vyema kwa wengine,” alisema Hamissi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mwakibete ameipongeza TPA kwa kuboresha huduma zake na kuongeza mapato huku akielekeza nguvu kubwa ielekezwe kwenye mifumo ya tehama.

Amesema ili kuendelea kupata matokeo chanya zaidi na bandari kufanya kazi kwa ufanisi ni muhimu kuwekeza kwenye teknolojia  zitakazowezesha mifumo ya tehama  itakayosaidia  kufuatilia kwa ufanisi utendaji wa shughuli za kila siku za bandari.

“Kaeni muone nini kinaweza kufanyika kuhakikisha mifumo ya tehama inakaa sawa na inafanya kazi kwa ufanisi, nchi kama China inafanikiwa kwa sababu bandari zake zina mifumo mizuri na bora,”amesema Mwakibete.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live