Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabomba mradi wa mafuta EACOP yawasili Dar

Mabomba Mafuta Eacop.jpeg Mabomba mradi wa mafuta EACOP yawasili Dar

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabomba ya mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda mpaka Chongoleani, mkoani Tanga, Tanzania (EACOP) yameanza kuwasili katika Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mabomba hayo jana Desemba 12, 2023 jijini Dar es Salaam, mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Safiel Msovu amesema zaidi ya mabomba 5,000 yamewasili nchini.

"Mradi uko tayari kuanza utekelezaji wa ujenzi. Nchi zote mbili zinahakikisha mradi unatekelezwa kama ulivyopangwa," amesema Msovu na kuongeza kuwa hatua za kuyasafirisha hadi maeneo ya mradi zinaendelea.

Amesema Serikali ya Tanzania kupitia TPDC inaendelea na uratibu wa mradi huo ikiwa imeshatoa takribani Sh500 bilioni kwa ajili ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa Msovu, mabomba hayo yaliyowasili yakiunganishwa urefu wake ni kilomita 100.

“Tumeanza utaratibu wa kuyasafirisha kutoka hapa Dar es Salaam mpaka Tabora ambako ndipo katikati na baadaye yatatawanywa kwenda maeneo mengine ya mradi," amesema Msovu.

Amesema kazi ya kuyachimbia ardhini mabomba itaanza Aprili, 2024 na ifikapo mwaka 2025 ujenzi wa mradi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100.

"Tunatarajia ifikapo mwanzoni wa 2026 mradi huu uanze rasmi shughuli ya kusafirisha mafuta kutoka Uganda kuja hapa nchini," amesema.

Kwa upande wake, Balozi wa Uganda nchini, Fred Mwesigye amesema hatua hiyo ni ya matumaini yanayoleta nuru kuelekea kukamilika kwa maono ya viongozi wa nchi hizo mbili.

"Tunamshukuru Mungu kwamba wananchi ambao wanapitiwa na mradi huu sasa wanakwenda kunufaika. Huu ndiyo uwajibikaji tunaoutaka, ni jukumu letu kuutimiza,” amesema.

Amewashukuru viongozi wanaohusika katika mradi huo kwa jitihada, uvumilivu na shauku yao ya kuona jambo hili linatimizwa.

Meneja Uendeshaji katika mradi huo, Stevan Miller amesema usafirishaji wa mabomba utafanyika kwa kutumia malori maalumu yaliyotengenezwa kwa ajili ya kazi hiyo.

"Malori haya yana urefu wa mita 18 ambao ndiyo urefu wa mabomba yaliyowasili nchini. Hii inafanya malori haya kuwa tofauti na mengine ambayo kwa kawaida yana urefu wa mita 12," amesema Miller.

Miller amesema madereva wa malori hayo wamepewa mafunzo maalumu yanayolenga

usalama barabarani, kukabiliana na dharura, mpango wa safari na kuzingatia kanuni za barabarani.

Amesema wamefunga mifumo maalumu itakayowezesha kutambua iwapo dereva ametumia kilevi au amechoka.

Kupitia mfumo huo, amesema iwapo dereva atakuwa amelewa gari halitawaka pale atakapoliwasha.

"Pia tunatumia teknolojia ya kisasa kunyanyua mabomba haya, ambayo hutumia mgandamizo wa hewa. Teknolojia inawezesha wafanyakazi kutokuwapo maeneo ya hatari wakati wa kunyanyua mabomba,” amesema.

Mkataba wa ujenzi wa bomba hilo ulitiwa saini April 11, 2021.

Mradi wa bomba la mafuta unatajwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 4 bilioni (Sh10 trilioni), kukamilika kwake kunatarajiwa kuiingizia Tanzania zaidi Sh4 bilioni kila siku.

Fedha hizo zitatokana na usafirishaji wa mapipa 200,000 kila siku yatakayokuwa yakitozwa Dola 12.2 (zaidi ya Sh24, 000) kila moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live