Serikali imetenga Sh. 20 bilioni kwa ajili ya kuyaendeleza mashamba makubwa, ikiwemo ya alizeti na michikichi, kwa ajili ya kuimarisha hali ya upatikanaji rasilimali za viwandani.
Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu katika uzinduzi wa awamu ya tatu ya ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera, uliofanyika leo Alhamisi, Juni 9, 2022.
Amesema, serikali imeanzisha sera ya kilimo cha mashamba makubwa, ambapo moja ya mkoa uliolengwa katika utekelezaji wa sera hiyo ni Kagera.
“Kagera mna ardhi nzuri kubwa, lakini haitumiki maeneo mengi yamebaki. Sasa tumekuja na sera ya kilimo cha mashamba makubwa. Moja ya mkoa tuliolenga kwa kilimo cha mashamba makubwa ni hapa Kagera. Serikali tumetenga bilioni 20 kuyaendeleaza mashamba,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema, mazao yatakayopewa kipaumbele ni alizeti na michikichi, ili kuisaidia nchi kupata malighafi za kutengeneza mafuta ya kupikia kwa ajili ya kupunguza changamoto ya upungufu.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali yake imedhamiria kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo hasa kwenye mazao ya chakula, ili kuifanya Tanzania kuwa muuzaji wa bidhaa za kilimo duniani, miaka 50 ijayo.
“Ni vyema kila mmoja kutambua kwa miaka 50 ijayo biashara itategemea sana kilimo na hasa mazao ya chakula dunia nzima. Hivyo hatuna budi kuifanya nchi yetu kuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa za kilimo na hivyo kuwa nchi bora ya kuuza nje bidhaa hizo,”amesema