Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa mabehewa mapya kwa ajili reli ya kisasa (SGR) ya Shirika la Reli Tanzania yanayotengenezwa na kampuni ya Sung Shin Rolling Stock (SSRT) iliyoko nchini Korea Kusini.
Ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2022 mara baada ya kutembelea kampuni ya SSRST inayotengeneza mabehewa na injini za treni nchini Korea Kusini ambapo amesema tayari mabehewa 36 kati ya 81 yamekamilika na yamekwishapelekwa Tanzania huku mabehewa 45 yaliyobaki yanategemewa kukamilika Machi 2023.
Kadhalika, Waziri Mkuu amemkaribisha nchini Rais wa Kampuni hiyo, Gye Shul Park kuja kuwekeza nchini Tanzania kutokana na fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo mpango wa Serikali wa kuendelea kuiboresha sekta ya usafiri wa reli.
“Mnakiwanda kikubwa, teknolojia ya hali ya juu pamoja na utaalamu na watalaam kwenye eneo hili. Kwa sasa tuna mipango mikubwa ya kuendelea kuiboresha sekta hii ya usafiri wa reli, yapo maeneo tofauti kwenye mpango wa kuunganishwa na reli ya kisasa (SGR), nakukaribisha kuja kuwekeza kitu kama hiki Tanzania,” amesema Majaliwa.